Ujumbe wa Kiongozi Muadhamukwa Mnasaba wa Kuzinduliwa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu
28/05/2016
Message to MPsAyatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ametoa ujumbe maalumu kwa mnasaba wa kuzinduliwa Majlisi ya Kumi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na huku akiwashukuru wananchi wa Iran kwa kujitokeza kwa wingi na kwa hamasa kubwa katika uchaguzi wa bunge, amewataka wabunge waliochaguliwa kufuatilia mambo ya lazima ya kufanikisha uchumi wa kimuqawama na kuimarisha na kustawisha utamaduni wa Kiislamu. Vile vile amewataka wajiweke mbali na mambo ya pembeni na ya kimirengo na kuzingatia zaidi maslahi ya umma. Aidha amewasisitizia kwa kuwaambia: Jukumu lenu la kimapinduzi na kisheria ni kulifanya bunge kuwa ngome madhubuti mbele ya njama na hila na ubeberu wa kijeuri wa waistikbari na liwe ni nguzo inayong'aa ya kutegemewa na wananchi waumini na wanamapinduzi.
Matini kamili ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambao umesomwa leo (Jumamosi) asubuhi na Hujjatul Islam Walmuslimin Mohammadi Golpeygan, Mkuu wa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu katika sherehe za ufunguzi wa Majlisi ya Kumi ya Ushauri ya Kiislamu ni kama ifuatavyo:

Bismillahir Rahmanir Rahim
Ninatumia fursa hii ya kuzinduliwa Majlisi ya Kumi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) tena katika mwezi wa Shaaban ambao ni mwezi wa umaanawi na kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu, mwezi wa idi na sikukuu kubwa za kidini, kutoa mkono wa kheri na fanaka kwa taifa lenye heshima na hadhi kubwa la Iran ya Kiislamu na kwenu nyinyi wabunge mliochaguliwa na wananchi na ambao mumebeba majukumu makubwa kama ambavyo ninaitumia fursa hii kutoa shukrani zangu nyingi sana kwa matabaka yote ya wananchi wetu azizi walioonesha hamasa ya kushiriki katika uchaguzi wa bunge na kuendeleza gurudumu lisilojua kusimama la utungaji sheria nchini, na kuongeza kongwa nyingine katika silisila na mnyororo huu muhimu sana. Yote hayo yamewezekana kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu na baraka Zake na rehema za Dhati Yake Tukukfu Ambaye kwa msaada Wake usio na mfano amelisaidia taifa la Iran, nchi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kupata taufiki hiyo. Moyo na ulimi hauwezi kubainisha kiwango kinachotakiwa cha shukrani kutokana na neema hiyo.
Kwa kushiriki kwa wingi mno wananchi wa Iran katika uchaguzi wenye umuhimu mkubwa wa Baraza la Kutunga Sheria (Bunge), kwa mara nyingine wametangaza utiifu na baia yao ya muda mrefu kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na wametoa majibu ya wazi kabisa kwa kila anayelitakia mabaya taifa hili. Uaminifu wenye thamani kubwa wa wananchi, unawataka viongozi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu katika sehemu mbali mbali walizo, watekeleze vizuri majukumu yao kama njia ya kushukuru neema hiyo. Jukumu letu viongozi hivi sasa ni kubwa sana kuliko huko nyuma.
Kiapo cha wabunge - ambacho watakitoa katika siku ya kwanza ya kufunguliwa bunge na ambacho ni kiapo cha kisheria kinachowawajibisha wabunge kutekeleza vilivyo majukumu yao - kimebainisha vipengee vya kimsingi vya majukumu ya wabunge bungeni; nanyi waheshimiwa mabibi na mabwana mnaweza kwa hekima na busara na ikhlasi na usafi wenu wa nyoyo, kufanikisha majukumu hayo kupitia utekelezaji wa kazi yenu ya kisheria - ambayo kimsingi ni ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wake - ili hatimaye muweze kupata heshima kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya wanadamu. Ni kwa kufanya hivyo ndipo Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu itakapoweza kuwa katika daraja na hadhi yake inayostahiki, yaani juu ya masuala ya nchi.
Hali ya tufani na kimbunga iliyopo katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kiujumla na chokochoko za kimataifa za mabeberru na vibaraka wao, ni mambo ambayo yameiweka Iran ya Kiislamu katika hali tata zaidi hivi sasa kuliko huko nyuma. Uwezo na nguvu za nchi za kukabiliana na hali hiyo, ni masuala ambayo yanahitajia kuwepo mwamko na imani ya kweli isiyotetereka na viongozi wote nchini kuwa na ubunifu wa kila namna. Jukumu la kimapinduzi na la kisheria mlilo nalo nyinyi waheshimiwa wabunge ni kuhakikisha kuwa Bunge linakuwa ni ngome imara mbele ya njama, kedi, makri na tabia ya mabeberu ya kupenda kujikumbizia kila kitu upande wake tena kijeuri na mhakikishe Bunge linakuwa ni nukta inayong'ara ya kutegemewa na wananchi waumini na wanamapinduzi.
Kufanikisha siasa za uchumi wa kimuqawama ukiwa na mambo yake yote ya lazima na yasiyokanushika na vile vile kufanya jitihada kubwa za kustawisha na kuimarisha utamaduni wa Kiislamu ni vipaumbele viwili vya haraka sana hivi sasa. Vipaumbele vingine viko katika sekta tofauti zinazohusiana na uwezo na nguvu za taifa, uimara wa usalama na kinga madhubuti kwa nchi, na vipaumbele hivyo ndivyo vitakavyodhamini kupatikana uadilifu wa kijamii na uhuru na maendeleo kwa nchi. Kutambua vyema vipaumbele hivyo ni miongoni mwa majukumu ya wabunge na ni vitu ambavyo wabunge wanaweza kuvielewa vizuri kwa akili zao erevu.
Ninawausia waheshimiwa wabunge kutawakali kwa Allah na kuwa na dhana nzuri kuhusiana na ahadi za Mwenyezi Mungu Muweza na kuwa na istiqama katika njia iliyonyoka ya Mwenyezi Mungu na pia napenda kukutahadharisheni na kushughulishwa na mambo ya ziada na ya pembeni ya kimirengo na kuzidiwa na misukumo binafsi badala ya maslahi ya umma.
Aidha ni wajibu wangu kuwashukuru kwa dhati ya moyo wangu, wabunge wa Bunge la Tisa na Spika wa bunge hilo kutokana na kazi zao kubwa kama ambavyo ninazishukuru kamati kuu za bunge na pia wote waliofanikisha uchaguzi wa Bunge la Kumi katika sekta zake zote.
Ninamkumbuka kwa wema Imam wetu mwenye hadhi kubwa (Imam Khomeini - quddisa sirruh) na mashahidi na watu wanaojitolea katika njia hiyo na sala na salamu ziende kwa Imam wetu wa Zama (Imam Mahdi AS) nikimuomba Mwenyezi Mungu akupeni nyote taufiki katika kila jambo lenu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
Sayyid Ali Khamenei
7 Khordad 1395
(Mei 27, 2016).