Hotuba ya Kiongozi Muadhamu katika Kumbukumbu ya Miaka 27 ya Kufariki Dunia Imam Khomeini MA
03/06/2016
The mourning ceremony on the 27th demise anniversary of Imam Khomeini (r.a) Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Ijumaa) amehutubia umati mkubwa uliojaa shauku wa matabaka mbali mbali ya watu katika Haram toharifu ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) iliyoko kusini mwa Tehran, na huku akisema kuwa, Imam alikuwa ni mwanachuoni muumini wa kweli, mchaji Mungu na mwanamapinduzi, amesisitizia wajibu wa kuendelezwa njia ya Imam mwanamapinduzi wa taifa la Iran ikiwa ndiyo njia pekee ya kuleta maendeleo na kufanikisha malengo ya wananchi na ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Vile vile amebainisha vielelezo vitano muhimu vya kuwa mwanapinduzi na kusema: Inabidi kuendelea na harakati na kufanya juhudi za kuiletea maendeleo nchi kwa kutumia uzoefu uliopatikana katika mazungumzo ya nyuklia, yaani kuthibiti udharura wa kutokuwa na imani na Marekani.
Katika hotuba yake hiyo aliyoitoa katika maadhimisho ya kukumbuka miaka ishirini na saba ya kufariki dunia Imam Khomeini (Rahmatullahi Alayh), Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, istilahi ya muumini mcha Mungu mwanamapinduzi ni ibara iliyokusanya kila kitu katika sifa alizokuwa nazo Imam Khomeini (quddisa sirruh) na kuongeza kuwa: Imam wetu mtukufu alikuwa ni muumini wa kweli wa Mwenyezi Mungu, muumini wa kweli wa watu, muumini wa kweli wa malengo yake na mumini wa kweli wa njia aliyotumia kwa ajili ya kufikia malengo.
Amma kuhusiana na sifa ya ucha Mungu ya Imam (Rahmatullahi Alayh), Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Imam alikuwa mja mwema wa Mwenyezi Mungu. Alikuwa mtu wa unyenyekevu, maridhia na mtu wa dua.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia sifa ya tatu maalumu aliyokuwa nayo Imam (quddisa sirruh) na kusema kuwa: Imam, alikuwa ni Imam mwanamapinduzi, na sifa hiyo ndiyo sababu kuu ya hasira za madola ya kimaada ya dunia.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa, madola ya kibeberu yanaliogopa mno neno Mapinduzi na kuwa Iran taifa la wanamapinduzi na kuongeza kuwa: Sababu kuu ya mashinikizo ambayo yamekuwepo dhidi ya taifa la Iran katika kipindi cha miaka mingi sasa kwa visingizio tofauti kama vile kadhia ya nyuklia na haki za binadamu, inatokana na woga huo huo wa madola ya kibeberu wa kuliona taifa la Iran na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu umejipamba kwa sifa ya uanamapinduzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia namna Iran ilivyotoka mikononi mwa madola ya kibeberu na kubadilika kuwa mfumo wa Kiislamu ambao ni kigezo kizuri kwa mataifa mengine duniani na kusema kuwa: Suala la kimsingi hapa ni kwamba, Imam mwanamapinduzi, ameiokoa Iran kutoka katika vinamasi vingi kama vinamasi vya kuwa tegemezi, ufisadi wa kisiasa, ufisadi wa kimaadili, kudhalilishwa kimataifa, kuzorota kielimu, kiuchumi na kiteknolojia na kuwa chini ya ubwana wa Marekani na Uingereza. Aidha amesema: Imam alileta mabadiliko makubwa sana katika njia ya harakati ya nchi na taifa na Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, Imam Khomeini (quddisa sirruh) alibadilisha reli ya harakati ya Iran na kuielekeza upande wa malengo makuu yaani utawala wa dini ya Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa: Utawala wa dini ya Mwenyezi Mungu una maana ya kuleta uadilifu wa kweli wa kijamii, kung'oa mizizi ya umaskini na ujinga, kung'oa mizizi ya unyonge na madhara ya kijamii, kujenga mfumo madhubuti wa thamani na matukufu ya Kiislamu, kudhamini usalama wa kimwili, kimaadili na kimaanawi, kuleta maendeleo makubwa ya kielimu nchini, kudhamini heshima na utambulisho wa kitaifa na vile vile nguvu za kimataifa na kuufanya uwezo wa kila aina ilio nao Iran utumike vilivyo kwa manufaa ya nchi na kwa sura inayotakiwa.
Aidha amesisitiza kuwa, Imam Khomeini (Rahmatullahi Alayh) kwa baraka za Mapinduzi ya Kiislamu alifanikiwa kuilekeza Iran upande wa ufanikishaji wa malengo hayo na kuongeza kuwa: Ijapokuwa ufanikishaji wa malengo hayo unahitajia muda wa kutosha na jitihada kubwa, lakini ni malengo yanayoweza kufikiwa na sharti pekee la ufanikishaji wake ni kudumu katika njia ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuwa wanamapinduzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameangalia kwa mamna fulani nakisi zilizopo katika mchakato wa harakati ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusema: Baada ya kufariki tunia Imam wetu mtukufu (Quddisa Sirruh), tumeweza kupata maendeleo katika nyakati ambazo tulifanya mambo yetu kimapinduzi, na kila pale tulipoghafilika na kutofanya mambo yetu kimapinduzi na kijihadi, tumeshindwa na tumebaki nyuma.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amewaambia wananchi wa mabataka tofauti kwamba: Inawezekana kufanya mambo kimapinduzi katika njia ya kufanikisha malengo hayo na iwapo hilo litatendeka, basi bila ya shaka yoyote maendeleo nayo yatapatikana na inawezekana pia kufanya harakati kwa mbinu nyingine tofauti na hiyo ya kimapinduzi, lakini wakati huo hatima itakuwa mbaya na taifa la Iran na Uislamu utapata pigo.
Amesema, Mapinduzi ya Kiislamu ni rasilimali bora na ya kipekee kwa taifa na nchi na kusisitiza kuwa: Kumetolewa gharama kubwa katika jitihada za kuyafanikisha Mapinduzi ya Kiislamu na kuyafikisha kwenye natija inayotakiwa, lakini pembeni mwa gharama hizo, kuna faida na manufaa mengi zaidi yamepatikana.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia uimara wa Mapinduzi ya Kiislamu baada ya kupita miaka 37 ya tangu yapate ushindi na kuongeza kuwa: Leo hii hali ya taifa la Iran inang'ara na iko wazi zaidi ikilinganishwa na huko nyuma na hivi sasa njia na fursa za kuepuka gharama hizo zimekuwa nyingi zaidi.
Vile vile amesisitiza kuwa: Mapinduzi ya Kiislamu yamepata ushindi kutokana na azma, irada na imani ya kweli ya wananchi na yamebakia imara hadi leo hii kwa nguvu hizo za wananchi na yameweza kusimama kidete mbele ya vitisho vya kijeshi na vikwazo bila ya kutetereka bali yameendelea mbele na harakati yake kiushujaa na kwa fakhari kubwa na katika siku za usoni pia yataendelea vivyo hivyo na harakati yake hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria kwamba, kuwa mwanamapinduzi hakuishii tu katika kipindi cha mapambano ya kufanya mapinduzi hayo na wakati wa Imam (Rahmatullahi Alayh) na kusema kuwa: Mapinduzi na kutenda mambo kimapinduzi ni jambo ambalo lipo muda wote, na mapambano ya ufanikishaji wa mapinduzi yalihusu kipindi maalumu na kwamba watu wote watakaofanya mambo yao kwa mujibu wa vielelezo vya kimapinduzi ni wanamapinduzi. hivyo hata vijana ambao hawakuwepo wakati wa harakati za Mapinduzi bali hata Imam hawakumuona, nao ni wanamapinduzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, fikra ambayo inauweka uanampinduzi sawa na misimamo mikali na ambayo inawagawa wananchi baina ya wenye misimamo mikali na wenye misimamo ya wastani, ni fikra potofu na kusisitiza kuwa: Kuleta fikra kama hizo ni kuwapa zawadi mabeberu na ni kukariri maneno yale yale ya maadui, hivyo fikra hiyo haipaswi kuruhusiwa kuingia katika utamaduni na misamiati ya kisiasa nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kosa jingine kuhusiana na suala la kuwa mwanamapinduzi na kutenda mambo kimapinduzi akisema: Ni kosa kutarajia kuweko kiwango kimoja cha uanampinduzi kati ya watu wote waliomo katika harakati na njia ya vielelezo na misimamo ya Mapinduzi, bali jambo la msingi linalopaswa kuzingatiwa ni vielelezo vya uanamapinduzi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kuna uwezekano mtu akawa na welewa mzuri kuhusiana na Mapinduzi ya Kiislamu na akafanya harakati zake na kutekeleza mambo yake kimapinduzi, na inawezekana kukawa na mtu mwingine akawashindwa kufanya mambo yake kwa uzito wa mtu huyu mwingine lakini wote hao wawili ni wanamapinduzi na hatuwezi kusema lazima kila mtu anayechunga vielelezo vya Mapinduzi ya Kiislamu lakini hafanyi harakati kwa uzito wa wanamapinduzi wengine, yeye si mwanamapinduzi au yuko dhidi ya Mapinduzi; hatuwezi kusema hivyo.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ameanza kubainisha vigezo vikuu vya mtu kuwa mwanamapinduzi, kutaja vielelezo vikuu vitano ambavyo ni: "kushikamana na misingi na thamani kuu za Mapinduzi ya Kiislamu," "kuhakikisha kuwa shabaha kuu muda wote ni malengo matukufu (ya Mapinduzi ya Kiislamu) na kutia hima kubwa ya kufikia kwenye malengo hayo," "kushikamana na kupigania vilivyo uhuru wa pande zote wa Iran," "kuwa na hisia kali mbele ya adui na kuacha kumfuata" na "kuwa na taqwa ya kidini na kisiasa."
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi kuhusu kielelezo cha kwanza cha kuwa mwanamapinduzi yaani "kushikamana na matukufu na usuli za kimsingi" na kuongeza kuwa: "kuwa na itikadi ya Uislamu sahihi mbele ya Uislamu wa Kimarekani" ndiyo nukta kuu na muhimu zaidi ya kielelezo hicho.
Vile vile amesema: Uislamu wa Kimarekani una matawi mawili, tawi la Uislamu wa fikra mgando, na tawi la Uislamu wa kisekulari, na kwamba ubeberu na uistikbari unaunga mkono aina zote hizo mbili za Uislamu (bandia na usio sahihi).
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, kuwa na itikadi na imani madhubuti ya kwamba wananchi ndio mhimili mkuu, ni msingi mwingine wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kwamba: Katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, msingi mkuu ni rai, matakwa, malengo na manufaa ya wananchi na kwamba kuwa na imani na itikadi ya kweli kuhusu mambo hayo ni jambo la dharura la kuwa mwanamapinduzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, maendeleo, mabadiliko na kujikamilisha ni miongoni mwa matukufu na mambo makuu ya thamani ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kwamba: Mtu mwanamapinduzi anayaamini pia matukufu hayo na muda wote huwa yuko katika mabadiliko na kupigania kuwa bora zaidi (kuliko jana yake).
Kuwasaidia wanyonge na matabaka ya watu dhaifu pamoja na kuwatetea na kuwahami watu wanaodhulumiwa duniani, ni matukufu mengine ambayo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyaashiria wakati akibainisha kielelezo cha kwanza cha kuwa mwanamapinduzi yaani kushikamana na usuli za kimsingi za Mapinduzi ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Kama kutakuwepo kushikamana huko ambako Qur'ani inakuita kwa jina la istiqama, basi harakati za viongozi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu mbele ya vimbunga vya matukio nayo itakuwa madhubuti na iliyonyooka, vinginevyo tutakumbwa na kufanya mambo kwa misimamo ya kuchupa mipaka na tutayumba. Aidha njia na muelekeo wa harakati yetu nao utakuwa unabadilika badilika kwa kila tukio linalotokea.
Baada ya hapo Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha kielelezo cha pili cha kuwa mwanamapinduzi yaani kuwa na hima kuu ya kujiletea maendeleo na kufikia kwenye malengo makuu matukufu na kuongeza kuwa: Tusisite hata mara moja kufuatilia malengo makubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu na ya wananchi na kamwe tusitosheke na hali tunayokuwa nayo, bali muda wote tufikirie kupiga hatua kubwa zaidi za maendeleo.
Amesema, katika upande wa pili wa kielelezo hicho kuna uvivu, uhafidhina na ukataji tamaa na kusisitiza kwamba: Njia ya maendeleo haina mwisho na tunapaswa muda wote kuendelea na njia hiyo kimapinduzi.
Kielelezo cha tatu cha kuwa mwanamapinduzi kilichozungumziwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba aliyoitoa mbele ya hadhara kubwa ya watu katika hauli ya 27 cha kukumbuka alipofaniriki dunia Imam Khomeini (Rahmatullahi Alayh) ni kushikamana na istiklali na uhuru. Kiongozi Mudhamu amekigawa kielelezo hicho katika vipengee vitatu vya kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi.
Ameongeza kuwa: Maana halisi ya istiklali na uhuru wa kisiasa ni kutotekwa na wala kuhadaiwa na mbinu mbali mbali zinaotumiwa na adui, na muda wote tuchunge uhuru wetu wa kisiasa wa ndani ya nchi, wa kieneo na wa kimataifa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria kwa mbali mbinu na hila zinazotumiwa na maadui hususan Marekani na kusema: Maadui hawaji na vitisho mara zote, bali baadhi ya wakati huja na tabasamu na vicheko na hata unaweza kuwasikia wakitoa matamshi kama ya kujipendekeza, kwa mfano watakuandikieni barua na wakwambieni, njooni tushirikiane kutatua matatizo ya dunia; sasa katika mazingira kama hayo, mtu anaweza kushawishika na kusema, kama ni hivyo, hilo ni jambo zuri, haya twendeni tukashirikiane na dola fulani la kibeberu kutatua masuala ya kimataifa; lakini mtu mwenye fikra kama hizo huwa ameghafilika kwamba, katika batini yake, adui huwa anatafuta kitu kingine kabisa na hicho anachokidhihirisha hadharani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Mwito wa adui wa kutaka kushirikiana na sisi kwa ajili ya kutatua masuala ya kimataifa una maana ya kumsaidia adui katika mchezo na medani aliyoiandaa yeye kwa ajili ya kutatua masuala maalumu anayoyataka yeye, (si kwamba ana nia njema kweli ya kutatua matatizo hasa ya dunia).
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa mfano mmoja wa wazi wa kuthibitisha suala hilo nayo ni kadhia ya Syria na kusema: Jambo ambalo lilitufanya tukatae kushiriki katika muungano wa Kimarekani wa eti kupambana na ugaidi katika kadhia ya Syria na masuala mengine mfano wake ni kwamba, tulishajua mapema kwamba walikuwa wana nia ya kutumia nguvu na ushawishi wetu na ushawishi wa nchi nyingine ili kufanikisha malengo yao maalumu, na si kupambana na ugaidi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ukumbusho wa kina akisema: Masuala kama hayo ambayo katika dhahiri yake hayakinzani hata kidogo na istikbali na uhuru wa nchi yetu, kivitendo yana maana ya kujaza jedwali la kazi za maadui, na kwa hakika ni kinyume kabisa na istiklali na uhuru wa taifa letu.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi kuhusu tawi la pili la kipengee cha istiklali na uhuru kwa kutilia mkazo umuhimu usio na mbadala wa uhuru wa kiutamaduni na kusisitiza kwamba: Kuwa mwanamapinduzi maana yake ni kutumia mtindo wa maisha ya Kiirani Kiislamu na kujiepusha kikamilifu na kuwaiga Wamagharibi na mabeberu.
Amesema, zana mpya zinazotumiwa na Wamagharibi katika mawasiliano ya kompyuta na Intaneti zinatumika kama "mhandisi wa taarifa" na silaha ya Magharibi ya kudhibiti tamaduni za mataifa mengine. Amesema: Tab'an zana hizo zinaweza kuwa na faida, lakini inabidi maaadui wapokonywe udhibiti wa zana hizo na ihakikishwe kuwa mawasiliano ya kompyuta na Intaneti hayawi chombo cha kujipenyeza adui na kudhibiti utamaduni wa taifa.
Istiklali na uhuru wa kiuchumi kwa maana ya kutoruhusu kumeng'enywa na nguvu za kimataifa ni nukta nyingine muhimu iliyobainishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kutolea ufafanuzi kielelezo cha tatu cha kuwa mwanamapinduzi yaani kushikamana na uhuru wa pande zote wa nchi.
Ameongeza kuwa: Baada ya mazungumzo ya nyuklia, Wamarekani walisema: Muamala wa nyuklia na Iran lazima upelekee kuingizwa uchumi wa Iran katika jamii ya kimataifa. Maana ya maneno hayo ni kuwa, Iran ikubali kumezwa na kumeng'enywe ndani na mpango na mfumo wa mabepari ambao kimsingi ni wa Wazayuni, mfumo ambao mabepari hao wameutunga duniani kwa ajili ya kudhibiti vyanzo vyote vya fedha vya dunia.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Katika vikwazo vyao, Wamarekani walikuwa na nia ya kuufanya kilema uchumi wa Iran, hivi sasa ambapo mazungumzo yamemalizika na kufikiwa natija, wanataka uchumi wa Iran umeng'enywe na uchumi wa dunia ambao tayari umeshamezwa na Marekani.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kwa kusisitiza kwamba, uchumi wa kimuqawama ndiyo njia pekee ya kuiwezesha Iran kuwa na uhuru wa kiuchumi na kuongeza kuwa: Kwa bahati nzuri serikali - kulingana na ripoti ilizotoa - katika mwaka huu wa Uchumi wa Kimuqawama, Hatua na Vitendo imeanza kuchukua hatua na kama itaendelea kwa nguvu hizi hizi, bila ya shaka yoyote wananchi wataona matunda yake mazuri.
Ameongeza kuwa: Katika maamuzi yote makubwa na katika kazi zote ikiwemo mikataba na nchi nyinginezo, lazima uchumi wa kimuqawama uwe ndio kigezo na kielelezo kikuu.
Ayatullah Udhma Khamenei amewakosoa watu ambao wanaona kuwa ustawi wa kiuchumi unaweza kupatikana tu kupitia uwekezaji wa kigeni na kusema: Kuvutia uwekezaji wa kigeni ni jambo zuri na la lazima, lakini lililo muhimu zaidi ya hilo ni kuufanya amilifu uwezo mwingi wa kila namna wa ndani ya nchi na kwamba si sahihi kukiegemeza kila kitu kwenye suala la kuvutia uwekezaji wa kigeni.
Vile vile ametumia mtazamo huo huo kuhusiana na teknolojia mpya na za kisasa akisisitiza kwa kusema: Kama nchi za kigeni zitatoa teknolojia hizo, si jambo baya, lakini kama hazikutoa, vijana wetu ambao wameifanya Iran azizi kuwa moja ya nchi kumi bora katika upande wa teknolojia za Nano, nyuklia na teknolojia nyinginezo, bila ya shaka yoyote wanao uwezo wa kuidhaminia nchi yao teknolojia yoyote ile inayohitajika, kama kutakuwa na mipangilio mizuri.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kielelezo cha nne cha kuwa mwanamapinduzi yaani kuwa na hisia kali mbele ya adui.
Amesisitiza kuwa: Inabidi kuifuatilia kwa kina na kuichunguza kwa undani kila harakati ya adui na iwe ni kama vile tuko katika medani ya vita ili tuweze kujua malengo yake na kukabiliana kwa hisia zinazotakiwa na sumu inayoweza kuwemo ndani ya harakati za adui na kujiwekea kinga madhubuti.
Aidha Ayatullah Udhma Khamenei amewakosoa watu ambao wanafumba macho yao mbele ya uadui wa kila aina, wa wazi na wa mara kwa mara wa Marekani, na badala yake wanaona kuwa ni kufanya njama dhidi yao kumzungumzia adui na kusema: Kuukana uadui mkubwa, wa kuendelea na wa wazi wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na dhidi ya taifa la Iran ni njama ambayo inafanyika kwa makusudi kwa lengo la kupungua hisia kali kuhusiana na shetani huyo mkubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, uadui na uhasama wa Marekani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ndiyo dhati ya Marekani na kuongeza kwamba: Mfumo wa kibeberu unadhihirisha tabia yake kupitia vita, kuunga mkono ugaidi, kuwakandamiza wapigania uhuru pamoja na kuwadhulumu, kuwanyanyasa na kuwakandamiza Wapalestina wanyonge na kwamba mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hauwezi kunyamaza kimya na kutoguswa na unyanyasaji na ukandamizaji huo.
Kiongozi Muadhamu amekitaja kitendo cha Marekani cha kuisaidia moja kwa moja nchi inayowashambulia kwa kila aina ya silaha wananchi wanyonge wa Yemen kuwa ni kushiriki katika mashambulizi na mauaji ya watu wasio na hatia na kusisitiza kwamba: Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, haiwezekani kunyamazia kimya jinai kama hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa muhtasari wa namna fulani wa hotuba yake hadi kufikia hapo akisema kwa kusisitiza kwamba: Mtu yeyote au mrengo wowote unaofanya kazi kwa ajili ya Uislamu na kwa jina la Uislamu, kama utaitegemea Marekani, basi mtu na mrengo huo ujue kuwa unafanya kosa kubwa na utapata pigo la kosa lake hilo.
Amekumbusha pia kuwa: Katika miaka hii hii ya karibuni pia, baadhi ya mirengo ya Kiislamu katika eneo hili iliamua kushirikiana na Wamarekani kwa madai ya kutumia akili ya kisiasa na kubadilisha mbinu, lakini hivi sasa mirengo hiyo inaona madhara ya kumuamini shetani mkubwa.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesema, Waingereza ni maafiriti na makhabithi zaidi kwa taifa Iran ikilinganishwa na maadui wengine na kuongeza kwamba: Hakuna hata wakati mmoja ambapo Waingereza wameacha uafiriti na ukhabithi wao dhidi ya taifa la Iran.
Ameongeza kwamba: Ni katika kuendelea uadui huo wa kila namna ndio maana taasisi ya kipropaganda ya serikali ya Uingereza katika hauli na kumbukumbu za mwaka wa kufariki dunia Imam wetu mtukufu ikashadidisha propaganda mbaya dhidi ya Imam wa taifa la Iran kwa kushirikiana na Wamarekani na kwa kutumia nyaraka bandia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, utawala fasidi wa Kizayuni ni miongoni mwa maadui wengine wa taifa la Iran sambamba na Marekani na Uingereza na kusisitiza kuwa: Inabidi tuwe na hisia kali katika kukabiliana na maadui na wakati maadui wanapotoa mapendekezo yoyote yale kama vile nakala za kisiasa na kiuchumi, inabidi tuchukue tahadhari kubwa kwani kama tutakuwa na hisia kali, jambo hilo litafuatiwa na kutomfuata adui na hiyo ndiyo hiyo "Jihadi Kubwa."
Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha kielelezo cha mwisho cha kuwa mwanamapinduzi yaani kuwa na taqwa ya kidini na kisiasa na kusema: Kuwa na taqwa ya kidini kuna maana ya kufaya jitihada kubwa za kuhakikisha kuwa malengo yote yaliyoainishwa na yanayotakiwa na Uislamu kwa ajili ya jamii yanafikiwa.
Vile vile amekumbusha kuwa: Katika suala hili hatupaswi kutosheka tu na mahesabu ya kiakili, kwani kufuatilia kivitendo malengo hayo ni wajibu wa kidini na kila mtu anayeutoa Uislamu kutoka katika maeneo ya kijamii na kisiasa, huwa hakuielewa dini tukufu ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi yua Kiislamu Ameongeza kwamba: Kama itapatikana taqwa ya kidini; taqwa ya kisiasa nayo itapatikana na itaweza kumlinda mtu kutokana na kuteleza kisiasa na na kumwepusha na kuyumba katika utekelezaji wa majukumu yake.
Sehemu ya mwisho ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya hadhara yenye shauku kubwa ya wananchi wa matabaka mbali mbali waliokusanyika kutangaza baia na utiifu wao kwa malengo matukufu ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) imehusiana na nasaha kadhaa mnuhimu ambapo nasaha yake ya kwanza ilikuwa ni kumzingatia Imam Khomeni (Rahmatullahi Alayhi) kuwa ni ruwaza na kigezo kamili.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuhusu suala hilo kwamba: Katika muongozo na ramani ya njia tuliyoichora leo hapa, Imam yuko juu ya kila kielelezo tulichokielezea na inabidi azingatiwe na apewe umuhmu mkubwa na kumfana kuwa ni kigezo kilicho kamili katika vielelezo vyote hivyo.
Amesema, kutaamali na kuzama muda wote katika kuzingatia sahifa ya Imam Khomeini na usia wake, na kuwa na ukuruba na mapenzi na maneo na misimamo yake ndiyo njia ya kumfanya kigezo cha kweli mwanachuoni huyo azizi aliyetangulia mbele ya Haki na amewausia watu wote na hususan vijana kulipa umuhimu mkubwa suala hilo.
Nasaha ya pili iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kutosahau uzoefu uliopatikana katika mazungumzo ya nyuklia.
Amesisitiza kwamba: Uzoefu huo unatufunza kwamba, hata kama tutaamua kulegeza misimamo mbele ya Marekani, kamwe Mmarekani hawezi kuachana na njama zake haribifu dhidi yetu.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia mazungumzo baina ya Iran na kundi la 5+1 na pia mazungumzo pembeni na moja kwa moja baina ya Iran na Marekani kuhusu kadhia ya nyuklia na kusema: Kwa jitihada za ndugu zetu amilifu, mazungumzo hayo yameweza kufikia kwenye nukta za pamoja lakini Marekani hadi hivi sasa inakataa kutekeleza ahadi zake na inaonesha si dola lenye mwamana kwa jinsi linavyokhalifu ahadi zake.
Ameongeza kuwa: Watu wengi walikuwa wanajua Marekani itafanya hivyo hata kabla ya mazungumzo ya nyuklia na walitabiri mapema jambo hilo, lakini baadhi ya watu walikuwa hawalijui hilo, hivyo sasa wanapaswa kuutambua vyema uhakika huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kama itatokezea - jambo ambalo ni muhali kutokea - tukawa na mazungumzo na Marekani katika suala lolote vile kama vile haki za binadamu, makombora, ugaidi, Lebanon, Palestina na jambo lolote lile na tukaamua kulegeza kamba katika misingi na misimamo yetu, tutambue vyema kuwa Mmarekani kamwe hawezi kulegeza kamba na baada ya vicheko na tabasamu na maneno haya na yale, Marekani itaendelea kupigania malengo yake bila ya kujali ahadi zake.
Nasaha za tatu zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni suala la umoja na mshikamano baina ya serikali na wananchi.
Ameongeza kuwa: Kila mtu katika nyakati tofauti anaweza akawa anavutiwa na serikali iliyoko madarakani au havutiwi nayo na tab'an jambo hilo halina tatizo lolote, lakini umoja na mshikamano baina ya wananchi na serikali haupaswi kuvurugwa kwa hali yoyote ile.
Ayatullah Udhma Khamenei Ameongeza kuwa: Tab'an kuikosoa na kuitaka serikali ifanye mambo wanayotaka watu ni jambo ambalo halina tatizo na wala suala hilo halikinzani na umoja na mshikamano, lakini kama ambavyo nimekuwa nikitoa nasaha hizi kwa kila serikai inayoingia madarakani, hapa narejea tena kusema kwamba tunapaswa kuwa macho, kusije kukazuka uhasama na chuki bali watu wote wanapaswa wafanye kazi bega kwa bega katika kukabiliana na vitisho na uadui wa maadui.
Amesisitizia pia haja ya kuweko umoja na mshikamano baina ya Mihimili Mitatu Mikuu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama) na kuongeza kwamba: Umoja haukinzani hata kidogo na kutekeleza kila mmoja majukumu yake kwa mujibu wa sheria, lakini hisia binafsi za kimirengo zisiruhusiwe kutia doa mshikamano na kufanya kazi kwa pamoja mihimili hiyo mitat mikuu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Inabidi kila mtu ajiepushe kutamka maneno ambayo yataleta mirengo miwili, kambi mbili na chuki na uhasama kati ya wananchi ili adui aione Iran nzima ni moja iliyoshikamana barabara.
Nasaha za nne zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kuyaangalia mapambano na Marekani kuwa ni kama medani ya vita.
Amekumbusha kuwa, tab'an Marekani ndiyo iliyoko katikati ya medani hiyo lakini uwanja wa mapambano umepanuka na kufika maeneo tofauti na baadhi ya wakati hata ndani ya Iran. Hivyo inabidi kuwa macho na kukabiliana vilivyo na harakati zote za matawi ya siri na ya dhahiri ya medani hiyo.
Kuhakikisha mipaka na maadui ni mipana na ni yenye rangi iliyokoza, ni nasaha za tano zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika maadhimisho ya miaka ishirini na saba ya kufariki dunia Imam Khomeini (quddisa sirruh).
Amesisitiza kwamba: Baadhi ya mirengo ya ndani ya Iran inaonekana imeghafilika na udharura wa jambo hilo na inashindwa kulinda mipaka yao na maadui na kwamba masafa yao na maadui hao ni dhaifu na yenye rangi hafifu. Amesisitiza kwa kusema: Kila mmoja anapaswa kuwa macho na kuhakikisha kuwa mistari ya mipaka yake na maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu na maadui wa Imam na wa taifa la Iran haiwi na rangi hafifu.
Nasaha za mwisho zilizotolewa na Ayatullah Udhma Khamenei katika maadhimisho hayo zimehusiana na wananchi na viongozi nchini. Amesema: Kuweni na imani kamili na nusra ya Mwenyezi Mungu na kuweni na yakini kwamba mustakbali bora ni wa taifa na wa vijana wa Iran hata kama maadui watachukia.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Hassan Khomeini, mfawidhi wa Haram ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) ametoa hotuba fupi na kusema kwamba Mapinduzi ya Kiislamu ni Mapinduzi ya Mwenyezi Mungu na ya wananchi. Amesema: Kuwa na uongofu wa Mwenyezi Mungu, heshima, mapenzi na huruma, umoja, nusra ya Mwenyezi Mungu na nguvu za wananchi ni katika sifa maalumu za kipekee za harakati adhimu na ya kihistoria ya Imam Khomeini na kwamba harakati hii imeendelea hadi leo hii kwa namna bora kabisa kutokana na jitihada kubwa zilizofanyika baada ya kufariki dunia Imam Khomeini kwa kuchaguliwa mtu anayefaa kabisa kushika nafasi yake.