Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Spika na Wabunge wa Bunge la Iran
05/06/2016

Photos: The chairman and the members of the 10th Majlis met with Ayatollah KhameneiAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumapili) ameonana na Spika na wabunge wa Majlisi ya Kumi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na kusisitizia ulazima wa kulindwa na kuhifadhiwa nguvu, haiba na nafasi ya bunge hilo, ambalo ni chombo kilicho juu ya masuala yote nchini Iran. Vile vile amegusia mambo ya lazima ya kuwezesha kutungwa sheria nzuri bungeni pamoja na vipaumbele vya bunge hilo katika masuala ya uchumi wa kimuqawama, utamaduni na siasa za ndani ya nchi, za kieneo na kimataifa na kuongeza kuwa: Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu inapaswa, sambamba na kupuliza roho ya utulivu nchini, iwe ya kimapinduzi na itunge sheria kimapinduzi na ioneshe radiamali madhubuti mbele ya misimamo ya kiuhasama na kiuadui ya Marekani kama ambavyo inapaswa pia kusimama imara katika kukabiliana na siasa za kiistikbari.

Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa pongezi kwa wabunge wa Bunge la Kumi kutokana na kupata taufiki ya kulitumikia taifa kupitia chombo cha kutunga sheria na kusema kuwa, nafasi ya mhimili huo wa dola ni kubwa na ni ya juu. Ameongeza kuwa: Jukumu la kutunga sheria la Bunge ni muhimu mno na kwa hakika ni sawa na kuweka reli ya kupitia gurudumu la kazi za serikali.

Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, jukumu la kusimamia mambo la Bunge halikinzani kivyovyote vile na suala la kushirikiana na serikali katika kazi zake na kuongeza kuwa: Ushirikiano huo hauna maana ya Bunge kuachana na haki zake kisheria na kwamba wabunge wana wajibu wa kutumia uwezo wao walio nao kikatiba kufuatilia utekelezaji mzuri wa sheria kama vile kufanya uchunguzi na uhakiki kuhusu mambo yanayofanywa na mihimili mingine ya dola.

Vile vile ameashiria kiapo cha wabunge cha kulinda misingi ya Uislamu na matunda ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Kwa hakika bunge lazima liwe juu ya mambo yote na kwamba jukumu la kulinda na kuhifadhi nafasi na haiba ya kweli ya Bunge ni la wabunge wenyewe.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, moja ya mambo yanayotoa dhamana ya kulindwa nafasi ya juu ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, ni bunge kujichunguza na kujitathmini lenyewe. Aidha amegusia suala la utungaji sheria nzuri na mambo ya lazima ya jambo hilo na kusema: Sheria zinazotungwa lazima ziwe na ubora, ziwe na umakini wa hali ya juu, ziangalie pande zote, ziwe wazi, zisikinzane na sheria nyinginezo, zipambane na ufisadi, ziendane na siasa kuu za nchi na chimbuko lake liwe ni mitazamo ya kiutalaamu ya watu waliomo serikalini na walioko nje ya serikali na ziwe na uwezo wa kulinda maslahi ya taifa na sio maslahi ya mahala fulani.

Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia muswada wa Mpango wa Sita wa Maendeleo ukiwa ni ajenda ya kazi za ziada na muhimu za bunge na kusema kuwa: Hali ya nchi hivi sasa ni hali ya kipekee na ya aina yake, hivyo mpango huo wa sita wa maendeleo unapaswa uchunguzwe na kujadiliwa kwa kina bila ya kubakisha utata wowote wala kudharau jambo lolote lile kabla ya kupasishwa kwake.

Ameashiria pia suala la kuingia katika Bunge la Kumi la Iran wabunge wengi wapya na kuongeza kwamba: Mimi ninalihesabu jambo hili kuwa ni fursa nzuri kwani kuingia bungeni wabunge wenye nguvu mpya na kushirikiana na baadhi ya wabunge wenye uzoefu kunaandaa uwanja wa kuundwa bunge lenye harakati nyingi na lenye msukumo mkubwa zaidi ambalo litatumia vizuri uzoefu wa wabunge wenye tajiriba ya kutosha bungeni humo.

Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameanza kutaja vipaumbele vya Bunge la Kumi la Iran na kusisitiza kwamba, uchumi, ni moja ya masuala muhimu sana yanayopaswa kupewa kipaumbele na bunge hilo. Ameongeza kuwa: Wabunge wana nafasi muhimu sana katika utekelezaji wa siasa za uchumi wa kimuqawama, kwani wanao uwezo wa kubadilisha mueleo wa hatua za kiuchumi za Serikali na kuzielekeza upande wa uchumi wa kimuqawama na halafu kuitaka serikali ifuate msimamo huo.

Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia njama za adui za kutumia silaha ya uchumi kwa ajili ya kutoa pigo kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusema kuwa: Ijapokuwa kuna baadhi ya mambo yamefanyika kiuanagenzi na baadhi ya misimamo ilichukuliwa kwa pupa na kuna na matamshi yalitolewa kwa hasira na hicho kumpa kisingizio adui cha kutumia silaha ya vikwazo, lakini inabidi matatizo ya kiuchumi yatafutiwe ufumbuzi wa maana hususan suala la kuzorota kasi ya kukua uchumi na suala zima la ukosefu wa ajira.

Amesema, utatuzi wa tatizo la kuzorota kasi ya ukuaji wa uchumi na kuandaa nafasi za ajira ni kulipa umuhimu mkubwa suala la uzalishaji wa ndani na hilo ni miongoni mwa vipaumbele vikuu na muhimu mno katika sekta ya uchumi. Amesisitiza kuwa, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unaona haya na kuingia soni kila unapoona kuna kijana hana kazi, lakini pia hali ya tahayuri anayokuwa nayo kijana asiye na kazi ndani ya familia yake ni kubwa zaidi, hivyo kuna wajibu wa kuchukuliwa hatua za maana na za kweli za kutatua tatizo hilo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kupambana na magendo ya bidhaa kuwa ni kipaumbele kikuu cha Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu katika suala la uchumi na kuongeza kwamba: Magendo ya bidhaa ni mithili ya jambia linaloupiga mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kutokea nyuma na ijapokuwa suala la kupambana na magendo hayo si jambo jepesi, lakini Serikali ina wajibu wa kukabiliana vikali mno na jambo hilo ovu, na kwa upande wake Bunge nalo linapaswa kuiunga mkono vilivyo Serikali katika jukumu hilo.

Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kusema kuwa, suala la utamaduni ni kipaumbele kingine muhimu kwa Bunge. Ameongeza kuwa, suala la uchumi ni kipaumbele cha haraka sana na cha sasa hivi kabisa, na suala la utamaduni ni la muda mrefu lakini umuhimu wake ni mkubwa zaidi kuliko suala la uchumi.

Ameongeza kuwa: Katika suala la utamaduni, kunaonekana aina fulani ya kuzembea na kutochukuliwa hatua zinazofaa na taasisi zinazohusiana na masuala ya utamaduni nchini, na kuna aina fulani ya ukosefu wa uwajibikaji katika uzalishaji wa bidhaa nzuri za utamaduni na kuzuia uzalishaji wa bidhaa zenye madhara ya kiutamaduni.

Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Baadhi ya wakati utaona kunasisitizwa suala la kujiepusha na kutumia bidhaa zenye madhara ya kiutamaduni kama vile baadhi ya vyakula, na mara nyingi masisitizo hayo huwa ni katika daraja ya tahadhari tu kuhusiana na bidhaa zenye madhara ya kiutamaduni wakati ambapo taathira mbaya za bidhaa hizo kwa watu ni hatari na ni kubwa zaidi na zinahitajia kuchukuliwa hatua kali dhidi yake.

Amesisitiza pia kuwa: Baadhi ya wakati utaona hata hakuchukuliwi misimamo wala hatua zozote za kukabiliana na uzalishaji au uingizaji wa bidhaa zenye madhara ya kiutamaduni nchini kwani watu wanaogopa kutuhumiwa kuwa wanakwamisha harakati ya uhuru wa upashaji habari.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia hatua kali zinazochukuliwa barani Ulaya na Marekani kwa ajili ya kudhibiti taarifa na upashaji habari na kusema kuwa: Sisi tunaogopeshwa na tuhuma zao zisizo na msingi kuhusiana na kukwamisha uhuru wa upashaji habari katika hali ambayo udhibiti wetu wa jambo hilo ni moja ya kumi ya hatua kali zinazochukuliwa na nchi za Ulaya na Marekani katika kudhibiti kuwafikia watu taarifa na habari.

Nasaha nyingine za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa wabunge wa Majlisi ya Kumi ya Ushauri ya Kiislamu ni wajibu wa kuwa wanamapinduzi, kubakia kuwa wanamapinduzi na kutenda mambo yao kiuanamapinduzi.

Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ni chombo cha kimapinduzi chenye chimbuko lake ndani ya Mapinduzi ya Kiislamu na amewalenga moja kwa moja wabunge hao katika matamshi yake akiwasisisitizia kwa kuwaambia: Katika kazi ya kutunga sheria na katika utekelezaji wa majukumu yenu kama wabunge na katika matamshi yenu na misimamo mnayochukua, kote huko mnatakiwa mufanye kiuanamapinduzi.

Aidha amesema, kuwa na misimamo ya pamoja wabunge kuhusiana na masuala makuu ya nchi ni jambo muhimu sana na huku akisifu kazi nzuri iliyofanywa na Bunge la Tisa katika upande huo amesema: Bunge linapaswa kuwa na msimamo ulio wazi na usiotetereka katika kukabiliana na mirengo ya kisiasa inayopinga Mapinduzi ya Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia vitimbi vya chuki za kupindukia vya Serikali na Baraza la Congress la Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa: Inabidi tuingie vilivyo katika medani ya kukabiliana na ujuba na jeuri za maadui na kutoa jibu kali ili wafumbe midomo yao, kwani adui katika upande wa kisiasa huwa anachukua hatua kulingana na majibu anayopata na kama ataona upande wa pili una tabia ya kuchukua maamuzi kwa pupa na kulegeza kamba kwenye misimamo yake, adui hutumia fursa hiyo kuzidi kuushinikiza na kuubana zaidi upande wa pili.

Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea kuzungumzia maudhui hiyo kwa kugusia mazungumzo ya nyuklia na kusema kwamba: Wamarekani wote, iwe ni serikali au Baraza la Congress au wagombea urais katika uchaguzi ujao, mara zote utawasikia wanatoa vitisho na kuonesha dhati yao ya kupenda kujikumbizia kila kitu upande wao na kwamba misimamo na vitisho vyao vya hivi sasa ni kama vile vilivyokuwepo kabla ya kufikiwa makubaliano ya nyuklia, hivyo hatupaswi kunyamazia kimya ujuba na jeuri yao hiyo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kutoa ufafanuzi kuhusu njama za ndani ya nchi za adui na namna anavyojaribu kutumia vibaya baadhi ya mambo ya ndani ya nchi na kusema kuwa: Adui anafanya njama ya kutumia masuala kama ya kikaumu, kiitikadi na kimirengo iliyopo nchini ili kujaribu kuzusha mivutano mikubwa ndani ya Iran, hivyo wabunge wanapaswa kuhakikisha kuwa njama hizo za adui zinafeli kikamilifu. 

Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesema: Mwakilishi Bungeni anaweza kwa mujibu wa mtazamo na fikra yake ya kisiasa kupiga kura ya kuunga mkono au kupinga jambo fulani, au kutoa maoni yake au kukosoa jambo fulani, na hilo halina tatizo lolote, lakini kila mmoja anapaswa achukue tahadhari na ahakikishe kuwa, ukosoaji au maoni na msimamo wake usije ukazusha hitilafu kama ilivyojiri katika baadhi ya nyakati kwenye mabunge ya huko nyuma na kuishia kwenye malumbano ya maneno, kushikana makoo na kuvutana vibaya.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuzusha fujo bungeni hupelekea ugomvi huo kuenea hadi katika jamii ya watu wa kawaida na kuongeza kuwa: Inabidi utulivu utawale Bungeni na iwapo utulivu huo utatawala bunge, bila ya shaka athari zake nzuri zitaenea pia katika jamii. 

Baada ya hapo, Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi kuhusu njama za adui katika upeo wa kieneo na kusisitiza kwamba: Adui anaendesha njama maalumu katika eneo nyeti ma muhimu sana la magharibi mwa Asia na anajaribu kuzivunja nguvu siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambazo ni kizuizi kikubwa mbele ya njama zake hizo.

Ameashiria pia baadhi ya sifa maalumu za eneo la magharibi mwa Asia kwa kusema: Kuweko Uislamu na Waislamu katika eneo hili, kuweko utajiri mkubwa wa mafuta na njia kuu za baharini na kuweko utawala wa Kizayuni katika eneo hilo ni katika mambo muhimu mno kwa adui na kwamba njama zinazoendeshwa hivi sasa na maadui hao kwenye eneo hili ndicho kile kitu ambacho walikitangaza katika miaka ya hivi karibuni kwa jina la kuundika "Mashariki ya Kati Mpya" na "Mashariki ya Kati Kuu."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia kufeli njama za Marekani katika eneo hili ikiwa ni pamoja na huko Iraq, Syria, Lebanon na Palestina kutokana na kusimama imara Jamhuri ya Kiislamu na kusisitiza kwamba: Inabidi tusimame kidete katika kukabiliana na siasa za kiistikbari na kufichua sura halisi ya mabeberu.

Vile vile ametahadharisha kuhusiana na kujiepusha na kuchukua misimamo na hatua zinazomfurahisha adui na kusisitiza kwamba: Hakikisheni kwamba uhakika na masuala ya kweli yanayohusiana na uistikbari na mfumo wa kibeberu vinakuwa ni vitu ambavyo mnavibainisha kwa uwazi katika maneno na misimamo yenu na chukueni tahadhari ili maneno na vitendo vyenu visije vikaisaidia Marekani na utawala wa Kizayuni kufanikisha malengo yao maovu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mwishoni mwa hotuba yake kwamba: Adui anafanya njama kubwa dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu katika upeo wa aina tatu; upeo wa kimataifa, upeo wa kieneo na upeo wa ndani ya nchi ambapo katika upeo wa kimataifa anaendelea kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; katika upeo wa kieneo anafanya njama za kuondoa vizuizi vinavyokwamisha njama zake na katika upeo wa ndani anafanya hila za kutia nguvu mambo ambayo anahisi yatamsaidia, hivyo mihimili yote nchini pamoja na viongozi na hususan wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, wanapaswa kuwa macho mbele ya njama hizo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameashiria kukaribia mwezi wa mtukufu wa Ramadhani ambao Waislamu huwa mgeni wa Mwenyezi Mungu ndani ya mwezi huo na kusema kuwa, mwezi huo ni fursa nzuri ya kukithirisha dua, kujijenga kiimani na kutenda mambo mema. Vile vile amesema kuwa, fursa ya kuwa mbunge katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu imekufikieni nyinyi wabunge wapendwa lakini fursa na nafasi hiyo ni ya kupita haraka, hivyo jueni thamani ya fursa hiyo na tieni hima ya kutekeleza majukumu yenu ya kisheria kwa kuomba msaada wa Mwenyezi Mungu.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Bw. Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amemkumbuka kwa kheri Imam Khomeini (quddisa sirruh) na kugusia vipaumbele na ratiba za Bunge la Kumi la Iran kwa kusema: Tuna jukumu na mas'uliya nzito ya kulinda ngome ya Mapinduzi ya Kiislamu na kwamba kitu ambacho kinaweza kulitoa eneo hili katika hali tata liliyo nayo na kulipeleka upande wa utulivu, utuvu na usalama wa kudumu, sambamba na kudumisha amani na usalama nchini Iran ni kuwa na mtazamo wa kimapinduzi na kuutekeleza kivitendo mtazamo huo.

Ameongeza kwamba, kuwa mwanamapinduzi ndiyo nukta kuu ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na kwamba Bunge la Kumi la Iran litafuatilia kwa karibu matukio ya eneo hili kwa hima na uzito mkubwa zaidi.  

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu amebainisha pia kwamba, vitimbi vinavyofanywa na Marekani baada ya makubaliano ya nyuklia vinaonesha kuwa uistikbari unataka kutoa pigo na kuyadhuru manufaa ya taifa la Iran na kusisitiza kwamba:  Wabunge wa wananchi nchini Iran wanatambua kwamba ni wajibu wao kulifanya bunge kuwa ngome madhubuti ya kulinda haki za taifa na kupambana vilivyo na mabeberu.

Bw. Larijani ameongeza kuwa, ushirikiano na kuamiliana vizuri Mihimili Mitatu Mikuu ya dola (Bunge, Serikali na Mahakama) pamoja na ushirikiano mzuri baina ya serikali na wananchi ni jambo la dharura sana hivi sasa na huku akibainisha kuwa, inabidi hatua za haraka zaidi na za makini zaidi zichukuliwe kwa ajili ya kuvuka katika kipindi hiki cha kuzorota kasi ya ukuaji wa uchumi ameongeza kwamba: Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu imeufanya uchumi wa kimuqawama na suala la kuimarisha uzalishaji wa ndani ya nchi kuwa ndio mhimili wake mkuu na kwamba uchumi huo unapewa kipaumbele cha kwanza katika kamati zote za Bunge na kwamba bunge hilo lina mipango na miswada maalumu inayotakiwa kwa ajili ya kusimamia ufanikishaji wa uchumi huo wa kimuqawama.