Kiongozi Muadhamu Ashiriki katika Mahfali ya kuwa na Mapenzi na Qur'ani Tukufu
07/06/2016
Leader at annual Ramadan Quranic meetingKatika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, mwezi iliyoshushwa ndani yake Qur'ani Tukufu, jioni ya leo (Jumanne) kumefanyika - kwa muda wa zaidi ya masaa matatu - mahfali na jalsa ya kuimarisha ukuruba na mapenzi na Qur'ani Tukufu, mahfali ambayo imehudhuriwa na Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Katika mahfali na jalsa hiyo iliyojaa nuru na kuhinikiza uturi na manukato ya kimaanawi ya Qur'ani Tukufu, maqarii na watu wanane waliohifadhi Qur'ani Tukufu pamoja na wahadhiri wa Qur'ani kutoka pembe zote za Iran wamesoma machache katika aya za maneno hayo matukufu ya Mwenyezi Mungu na kikundi kimoja cha kusoma Qur'ani kwa pamoja kimepata fursa pia ya kusoma machache kutoka katika kitabu hicho kitakatifu.
Katika jalsa na mahfali hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, ujamali wa maneno ya Qur'ani ni muujiza na ni dirisha la kuvutika watu upande wa kuelewa vizuri mafundisho aali na yenye maana pana ya aya za Kitabu hicho kitukufu. Aidha ameelezea ulazima wa kupewa umuhimu jalsa na vikao vya Qur'ani katika kona zote za Iran na kugusia namna dunia leo hii inavyohitajia mno mafundisho ya Qur'ani Tukufu kuliko jambo jingine lolote na kuliko wakati mwingine wowote na kusema: Kama maana pana za Qur'ani Tukufu watabainishiwa watu kwa lugha nyepesi ya kisasa bila ya shaka yoyote taathira za aya hizo zitakuwa kubwa na zitaandaa uwanja wa kupatikana maendeleo ya kweli ya mwanadamu, kwani heshima, nguvu na uwezo, ustawi wa kimaada, kuimarika kimaanawi, kuenea fikra na itikadi na kupatikana furaha na utulivu wa moyoni, yote hayo yanategemea kiwango cha kushikamana kwetu kivitendo na mafundisho ya Qur'ani Tukufu.
Mwanzoni mwa matamshi yake, Ayatullah Udhma Khamenei amewakumbuka kwa wema maqari na wasomaji wa Qur'ani Tukufu waliotangulia mbele ya Mwenyezi Mungu mwaka jana katika maafa ya Mina huko Saudi Arabia na sambamba na kuelezea kufurahishwa kwake kwa kuona kuwa vijana wanazidi kushikamana na Qur'ani nchini Iran amesema kuwa: Ijapokuwa ujamali na mvuto wa maneno ya Qur'ani Tukufu ni muujiza, lakini lengo la maneno hayo ni kufungua dirisha la kufikia kwenye anga iliyojaa baraka ya mafundisho ya Qur'ani.
Amesisitiza kwamba: Kama mafundisho ya Qur'ani Tukufu yatapewa umuhimu unaotakiwa, bila ya shaka yoyote kina na maana pana za aya za Qur'ani na taathira zake zitakuwa kubwa zaidi katika dunia ya leo iliyo na mazonge mengi na inayokabiliwa na tufani za matatizo na mashaka ya kila namna.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuongezeka na kuenea na kuimarika zaidi jalsa na mahfali za Qur'ani Tukufu nchini Iran kuliko ilivyokuwa kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu bali hata katika kipindi cha mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni jambo lenye ibra na maana maalumu na kuongeza kuwa: Moja ya mambo ya lazima yanayopaswa kufanyika nchini, ni kuenezwa na kuimarishwa zaidi vikao vya kusoma na kusikiliza Qur'ani Tukufu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kama vinavyofanyika vikao vya maombolezo na vya furaha kuhusiana na Ahlul Bait (Alayhimus Salaam), vikao vya Qur'ani Tukufu navyo inabidi vienezwe na kuimarishwa zaidi ili sambamba na kufanyika jambo hilo, iweze kuongezeka kasi ya ustawi na ukuaji wa suala zima la kushikamana na mafundisho ya Qur'ani Tukufu.
Vile vile amegusia namna dunia ilivyo na pengo la utambulisho, fikra na imani na jinsi mwanadamu anavyohitajia mno mafundisho ya Qur'ani Tukufu kuliko wakati mwingine wowote na kusisitiza kwamba: Inabidi tuiimarishe zaidi na zaidi misingi yetu ya kiimani na kuwa na welewa wa kutosha kuhusiana na lugha inayofaa ya kuyafikia kwa njia sahihi mafundisho ya Qur'ani Tukufu kwa watu wengine ili kwa njia hiyo tuweze kuyatangaza vizuri mafundisho ya Kitabu hicho kitukufu cha Mwenyezi Mungu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kama mafundisho ya Qur'ani Tukufu yatafikishwa vizuri kwa watu, bila ya shaka yoyote yatakuwa na taathira nzuri na kubwa sana duniani na wakati huo tena madola ya kibeberu na silaha zao pamoja na utawala wa Kizayuni hawataweza kufanya ghalati na upuuzi wowote ule.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema pia kuwa, utulivu wa kiroho na kidini ni miongoni mwa baraka nyingi za kuwa na welewa wa kutosha kuhusiana na mafundisho ya Qur'ani Tukufu na kuongeza kwamba: Utulivu huo ndio unaoandaa uwanja wa kuongezeka imani ya mtu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwa uwezo na nguvu zisizo na kikomo za Allah.