Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Washairi na Watu wa Utamaduni na Fasihi
21/06/2016
Leader meets with poetsMajimui ya watu wa utamaduni, wahadhiri wa tungo na fasihi ya Kifarsi, washairi chipukizi na majimbi wa Iran pamoja na malenga kadhaa kutoka katika nchi za Pakistan, India na Afghanistan wameonana na Ayatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika usiku wa kuamkia siku ya kukumbuka kuzaliwa "Karim Ahlul Bait" Imam Hassan al Mujtaba (Alayhis Salaam).
Katika mkutano huo, Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, malenga na washairi ni hazina na ni rasilimali yenye thamani kubwa kwa Iran na huku akisisitizia ulazima na wajibu wa tungo kuwa hai, kuwa na maudhui zinazokwenda na wakati, zinazoandikwa kwa wakati mwafaka pamoja na kuwa na misimamo imara kuhusiana na masuala makuu na mahitaji ya nchi, amesema: Leo hii kuna vita vingine vinaendelea duniani viitwavyo vita laini na mapambano ya kisiasa na kiutamaduni hivyo tungo za kishairi zinapaswa kutumika vizuri mno katika kukabiliana na mashambulizi yanayotokana na vita hivyo laini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine tena amemuenzi marhum Hamid Sabzevari, jimbi aliyebobea katika tungo na aliyekuwa mahiri na bingwa wa mashairi ya kila namna pamoja na hazina kubwa ya maneno ya lugha aliyokuwa amehifadhi kichwani, ni katika sifa za pekee za jimbi huyo wa fasihi. Ameongeza kuwa: Sifa ya kipekee ya marhum Sabzevari, ni mashairi yake yaliyoleta taathira kubwa, yaliyokuwa na ubora wa hali ya juu na yaliyokwenda na wakati.
Ametumia fursa hiyo kusema pia kuwa, mashairi ya kuimbwa ni katika mashairi yenye taathira kubwa. Amesema: Kasi na kuenea haraka kwa watu wengi mashairi ya kuimbwa, ndiko kunakoyafanya mashairi ya aina hio kuwa na taathira kubwa zaidi kati ya mashairi yote na huwa ni mithili ya hewa mpya inayopulizwa na kupenya katika jamii; hivyo inabidi kutunga kwa wingi mashairi mazuri ya aina hiyo na kuyasambaza kwa njia sahihi ili kujaza pengo lililo wazi katika uga huo.
Baada ya hapo, Ayatullah Udhma Khamenei ameanza kubainisha nafasi na jukumu la mashairi kwa kusema kuwa malenga na washairi ni sehemu ya rasilimali azizi zaidi na ya kujivunia zaidi nchini Iran. Ameongeza kuwa: Rasilimali hiyo inabidii iingie katika medani na kukidhi mahitaji yanayotakiwa na nchi katika nyakati muhimu na zinazofaa kabisa na kila wakati yanapozuka masuala kama ya kisiasa, kiutamaduni, mahusiano baina ya watu na mifungamano ya kijamii na kushiriki vilivyo katika vita vya kupambana na maadui wa nje.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Shairi inabidi liwe hai na linapaswa lioneshe msimamo wake kuhusiana na masuala yaliyopo wakati wa kutungwa kwake na liwe ni lenye kukidhi mahitaji ya nchi yetu.
Vile vile amesisitizia wajibu wa kuenezwa kwa kiwango kikubwa mashairi na nyimbo hai zenye maudhui za maana kama ambavyo amehimiza pia jukumu kubwa la Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB na vyombo vingine husika katika kadhia hiyo na kuongeza kuwa: Leo hii mashairi hai na muhimu sana kama vile mashairi yanayohusiana na Palestina, Yemen, Bahrain, vita vya kujihami kutakatifu (vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi mfumo mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran), mashairi kuhusu mashahidi wapiga mbizi na mashahidi wa kulinda Haram au maudhui kuhusu dhulma wanazofanyiwa watu wanaopigana jihadi kama vile Sheikh Zakzaki, sheikh madhlumu, shujaa na mwenye misimamo isiyoyumba wa Nigeria ni muhimu sana kuliko wakati wa huko nyuma, lakini cha kusikitisha ni kuona kuwa, mashairi muhimu kama hayo ambayo yana taathira kubwa na zenye kuleta mwamko na kuimarisha nyoyo, hayasambazwi wala kuakisiwa vile inavyotakiwa, bali kuna nuksani na kutofanywa kazi ipasavyo katika uga huo.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amelitaja jukumu la kubainisha usaliti wa Wamarekani katika suala la makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa baina ya Iran na kundi la 5+1 maarufu kwa jina la JCPOA kuwa ni uwanja mwingine ambao malenga wanaweza kuutumia kutunga tungo muhimu na hai na kusema kuwa: Mbali na wanasiasa, wasanii na hususan malenga na washairi wana wajibu wa kuzifikishia vizuri na inavyopasa fikra za walio wengi masuala hayo ya uhakika.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekosoa baadhi ya hatua ghalati na zisizo sahihi za kuwakuza na kuwaenzi wasanii ambao hawana maadili mazuri wala hawana imani na kuongeza kwamba: Cha kusikitisha ni kuwa baadhi ya wakati utaona wasanii hao hawajawahi kuonesha mapenzi wala hisia zozote zile kwa Uislamu na kwa Mapinduzi ya Kiislamu, lakini wanaenziwa, halafu hapo hapo kuna wasanii ambao umri na rasilimali yao yote ya kisanii wameitumia katika njia ya Uislamu na ya Mapinduzi ya Kiislamu, lakini hawaenziwi bali wanapuuzwa na kusahauliwa.
Nasaha nyingine zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano huo ni kutumiwa vizuri fursa ya mapenzi ya wananchi na vijana kwa mashairi yenye faida nyingi kama vile mashairi ya kidini ya huzuni na maombolezo.
Amegusia mifano ya mashairi ya majonzi na simanzi yenye maana pana na namna yalivyotumika vizuri katika kipindi cha kupambana na utawala wa taghuti kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na vile vile kwenye kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu na kusisitiza kwa kusema: Tab'a medani na aina ya vita vya leo inatofautiana na medani na vita vya wakati wa mapambano na utawala wa taghuti na kipindi cha mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini, kwani hivi sasa tuko kwenye medani ya vita laini na vita vya kisiasa, kiutamaduni na kiusalama, na vita vya kukabiliana na njama za maadui za kujipenyeza na kutafuta ushawishi nchini Iran. Aidha amesema: Katika medani ya vita vya hivi sasa, fikra misimamo na maamuzi, ndiyo mambo yanayopambana na kwamba moja ya silaha kuu na muhimu katika vita hivyo ni silaha ya tungo za kishaidi.
Amesisitizia pia muhumi wa "kutungwa, kutarjumiwa na kusambazwa kimaudhui mashairi muhimu katika masuala kama vile Palestina, vita vya kujihami kutakatifu, hali ya eneo la Mashariki ya Kati na Yemen," "kubadilisha maana na maneno aali ya dua mbali mbali na matini za kidini na kuziingiza katika mashairi" pamoja na "kusoma mashairi ya kidini yenye maana pana na nzito kwa shabaha ya kufikisha na kusambaza mafundisho ya Maimamu maasumu (Alayhimus Salaam)," ndizo zilizokuwa nasaha za baadaye za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano huo uliojaa mapenzi na kushibana.
Vile vile Ayatullah Udhma Khamenei amesisitizia udharura wa kuimarishwa na kustawishwa kiubora mashairi na washairi kutosita hata chembe katika mahala fulani, bali muda wote wafikirie kujiendeleza zaidi na kuongeza kuwa: Kuna haja ya kuimarishwa na kuungwa mkono majimui za wananchi na za kitaalamu kama vile wilaya ya fasihi kama njia ya kuimarisha na kukuza mashairi na kulea washairi wapya.
Mwanzoni mwa mkutano huo, malengo 23 wamesoma tungo zao mbele ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Vile vile malenga na washairi hao wamesalishwa sala za Magharibi na Isha na Ayatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na baadaye kula futari pamoja naye.