Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Mkuu na Maafisa wa Chombo cha Mahakama
29/06/2016
Leader meets with Judiciary OfficialsAyatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo jioni (Jumatano) ameonana na mkuu na maafisa wa chombo cha mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa, miongoni mwa majukumu makuu na lengo hasa la chombo hicho ni kufanya jitihada zisizochoka za kuvutia ridhaa ya wananchi kwa mujibu wa mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Vile vile amegusia kukaribia Siku ya Kimataifa ya Quds (Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani) na kusisitiza kuwa: Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, siku ya Ijumaa, kwa mara nyingine tena, kutasikika sauti moja ya kuwatetea wananchi madhlumu wa Palestina katika kona zote za Iran na ulimwengu mzima wa Kiislamu na Inshaallah umma wa Kiislamu utatekeleza kivitendo faradhi hii muhimu ya kuwalinda na kuwahami wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemuenzi na kumtaja kwa wema shahid Ayatullah Beheshti mwasisi wa Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa, shahid Beheshti alikuwa kiongozi mwenye fikra pana, asiyetetereka katika misimamo yake, mwenye tadibiri, mchapa kazi na mfuatiliaji wa mambo, na amewashukuru kwa udhati wa moyo wake, maafisa, viongozi na wafanyakazi wa chombo hicho kwa jitihada zao za kuhakikisha wanatekeleza vilivyo majukumu yao.
Vile vile amemsifu mkuu wa hivi sasa wa chombo hicho na kusema kuwa ni mwanachuoni alimu, mja mwema na aliyebobea katika elimu na kuongeza kuwa: Chombo cha Mahakama nchini Iran kina umuhimu mkubwa sana kutokana na majukumu yake kama vile kusimamia utekelezaji wa sheria, kuzuia vitendo vya uhalifu na pia kutokana na mkuu wa chombo hicho kushiriki katika vikao vya mabaraza makuu na ya asili ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ambayo yana taathira ya moja kwa moja katika siasa kuu za Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kutokana na umuhimu wake huo wa kupigiwa mfano na hatua na vitendo vya Chombo cha Mahakama nchini Iran vimekifanya chombo hicho daima kuwa ni chombo nyeti sana na ni kwa sababu hiyo pia ndio maana chombo hicho kinasakamwa mno katika mashambulizi na propaganda kubwa sana za maadui.
Ameongeza kuwa: Propaganda za upotoshaji za vyombo vya habari vya kibeberu dhidi ya Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimeongezeka zaidi hivi sasa na sababu yake ni misimamo ya kimapinduzi, ya wazi na yenye thamani ya mkuu wa chombo hicho na maafisa wake wa ngazi za juu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitizia wajibu wa chombo hicho kuvutia ridhaa ya wananchi likiwa ni jukumu la Kiislamu na shabaha yake kuu na ya kimsingi na kusema kuwa, kulinda usalama wa Chombo cha Mahakama ndiyo njia bora zaidi ya kuvutia ridhaa za wananchi na kuongeza kwamba: Kuna wajibu kwa Chombo cha Mahakama kuwafuatilia kwa nguvu zote na kwa uzito wa hali ya juu na bila ya kutetereka, wahalifu na mafisadi katika mikoa na miji yote na ihakikishwe kuwa jambo hilo linaendelea.
Aidha amewalenga moja kwa moja maafisa wa chombo hicho cha mahakama kwa kuwaambia: Usalama wa Chombo cha Mahakama ni jambo lenye umuhimu wa juu kabisa na mnapaswa kulihesabu jambo hilo kuwa ndilo jukumu lenu la kimsingi.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesisitizia udharua wa kueleweshwa wananchi kuhusu namna chombo hicho kinavyokabiliana na wahalifu hata ndani ya chombo cha mahakama chenyewe.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kuna baadhi chache ya watu ndani ya chombo hicho hufanya uhalifu na vitendo vilivyo kinyume na sheria, watu hao mbali na kuwasaliti viongozi na wafanyakazi wenzao wanaofanya kazi kwa ikhlasi na kwa juhudi kubwa ndani ya Chombo cha Mahakama, huwa wanawadhulumu pia wananchi kwa vitendo vyao hivyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameyataja masuala kama kuwa na mipangilio iliyosimama juu ya mihimili na nyakati maalumu kwa ajili ya kutekeleza mipango ya chombo hicho na kuzuia vitendo vya uhalifu sambamba na kufanyia marekebisho ni mambo mengine ya lazima yenye umuhimu mkubwa sana kwa Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ambayo yana matunda mazuri kwa chombo hicho. Vile vile amesisitizia kwa mara nyingine ulazima wa kupunguzwa adhabu za vifungo jela na kusema: Inabidi chombo hicho kitume watu wataalamu wenye uzoefu na wanafikra kwa ajili ya kuwa na mipangilio mizuri ya kutoa adhabu zisizo za vifungo jela.
Aidha amesema kuhusiana na udharura wa kuzuia kutokea vitendo vya uhalifu kwamba: Jambo hilo ni muhimu mno na halihusiani tu na Chombo cha Mahakama na linahitajia pia fikra, elimu na uzoefu kulitekeleza.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, moja ya kazi za dharura kabisa kwa Chombo cha Mahakama ni kuakisiwa kazi cha chombo hicho katika vyombo vya habari ili wananchi waelewe ni kazi gani zinafanywa na chombo hicho. Amesema: Inabidi wananchi waeleweshwe kazi nzito na ngumu zinazofanywa na Chombo cha Mahakama kupitia mbinu mbali mbali mpya na zenye mvuto za vyombo vya mawasiliano ya umma na vya upashaji habari.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, kupewa wananchi mafunzo yenye mvuto kuhusu masuala jumla ya kisheria na kimahakama kutapelekea kupungua idadi ya watu wanaokwenda mahakamani na amewausia maafisa wa mahakama walipe uzito wa hali ya juu suala la kuandaa mazingira ya kuweza wananchi kufaidika na ushauri wa kimahakama wa masaa 24.
Vile vile amesema ni jambo la dharura kwa Chombo cha Mahakama kufuatilia kisheria masuala ya kimataifa na kuongeza kwamba: Suala la kufuatilia haki za taifa la Iran zilizoporwa kutokana na vikwazo, linapaswa kuwa ajenda ya chombo hicho cha mahakama.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia hukumu iliyotolewa na mahakama za Marekani za kuzuia mali za taifa la Iran kwa madai ya kipuuzi na tuhuma zisizo na msingi na kusema kwamba: Kuporwa haki za taifa la Iran kupitia vikwazo ni suala ambalo linapaswa kufuatiliwa kisheria katika upeo wa kimataifa.
Suala la kufuatilia haki za maelfu ya wahanga wa vitendo vya ugaidi vilivyotokea nchini Iran, kufungua kesi dhidi ya tawala ambazo zinawaunga mkono kwa siri na kwa dhahiri pamoja na kuwapa hifadhi wauaji wa wahanga hao na suala la kulindwa kisheria shakhsia muhimu wa Kiislamu wanaodhulumiwa katika kona mbali mbali za dunia ni nasaha nyingine ambazo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekiusia Chombo cha Mahakama cha Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesema, suala la kuhuisha haki za binadamu za Kiislamu katika upeo wa kimataifa ni jukumu jingine la Chombo cha Mahakama cha Iran na kuongeza kuwa: Haki za binadamu zinazodaiwa kupiganiwa na Magharibi zimesimama juu ya misingi mibovu na ghalati na kuna wajibu wa kubainishiwa walimwengu na jamii za kisheria duniani jambo hilo na kufuatiliwa kimataifa haki za binadamu za Kiislamu zilizosimama juu ya misingi makini na kimantiki.
Amesema ni aibu kubwa kwa Umoja wa Mataifa kutangaza hadharani kuwa umelazimika kufumbia macho jinai na mauaji ya watoto wadogo yanayoendelea hivi sasa nchini Yemen kwa kuhofia kunyimwa misaada ya fedha na baadhi ya nchi na kuongeza kuwa: Aibu na kashfa hiyo ndio uvunjanji wenyewe wa haki za binadamu na tuna wajibu wa kulifuatilia kimataifa, kisheria na kimahakama jambo hilo.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa muhtasari wa namna fulani wa matamshi yake kwa kusisitiza kuwa: Chombo cha Mahakama cha Iran kinapaswa kufuatilia na kufanya mambo yake yote kimapinduzi.
Amesema: Tab'an, tofauti na propaganda za baadhi ya watu, suala la kufanya kazi kimapinduzi halina maana ya kuwa na misimamo mikali, bali kufanya mambo kimapinduzi kuna maana ya kufanya kazi kiuadilifu, kwa hekima na busara kubwa, kwa umakini, kwa kuwa na uchungu, kiinsafu, kutotetereka na kutomuonea muhali mtu yeyote yule.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Amoli Larijani, Mkuu wa Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti fupi kuhusu hatua muhimu zaidi zilizochukuliwa na chombo hicho.
Ayatullah Larijani aidha amesema, wigo wa kazi za chombo hicho ni mpana sana. Amesema, chombo hicho kilifuatilia zaidi ya kesi milioni 14 katika mahakama na kwenye mabaraza ya kutatua hitilafu kama ambavyo kilitoa huduma zaidi ya milioni 70 zilizoorodheshwa katika mwaka uliopita.
Mkuu wa Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema kuwa, masuala kama kushadidisha usimamiaji wa utendaji kazi majaji na wafanyakazi wa chomo hicho pamoja na kulipa uzito wa hali ya juu suala la kupambana na ufisadi kwa ajili ya kudhamini usalama wa chombo hicho cha mahakama ni hatua nyingine zilizochukuliwa hadi hivi sasa. Ameongeza kuwa: Kupambana na ufisadi wa kiuchumi kwa nguvu kubwa na bila ya kumuonea muhali mtu yeyote ikiwa ni pamoja na kufuatilia kesi za watuhumiwa wa mafuta na kesi za madeni makubwa katika benki na vile vile kuandaa mazingira ya kuweko usalama wa kiuchumi kwa ajili ya sekta ya uzalishaji bidhaa na uwezekezaji nchini Iran ni miongoni mwa siasa na hatua muhimu zaidi zilizochokuliwa na chombo hicho cha mahakama.
Vile vile Ayatullah Amoli Larijani amegusia masisitizo ya mara kwa mara ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu wajibu wa kupunguwa idadi ya watu wanaofungwa jela na kusema: Kumeandaliwa ajenda makini na iliyozingatia pande zote kuhusu suala hilo na hivi sasa chombo hicho kinafuatilia suala la kutoa adhabu zisizo za kifungo jela na hivi sasa idadi ya watu wanaohukumiw'a kufungwa jela imepungua kwa asilimia 20 nchini.
Mkuu wa Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vile vile ameashiria kazi zilizofanywa na chombo hicho katika upande wa kuzuia kutokea vitendo vya uhalifu, ratiba zilizosimama kwenye mihimili maalumu na kusafishwa na kufanyiwa marekebisho sheria nchini na kuongeza kuwa, miongoni mwa matatizo yanayokikabili chombo hicho ni bajeti ndogo na pia ukosefu wa nguvu kazi ya kutosha.