Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wanachuo
03/07/2016

Leader meets with university studentsWanachuo zaidi ya elfu moja wakiwemo wawakilishi wa jumuiya mbali mbali za wanafunzi wa vyuo vikuu, Alasiri ya siku ya Jumamosi walionana na Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mazingira yaliyojaa mapenzi na kushibana kwa muda wa takriban masaa matano na kutoa dukukuduku zao kuhusu mazingira yao ya kiuanafunzi, pamoja na dukuduku za kiutamaduni, kiajamii, kisiasa na kiuchumi za jamii ya vijana nchini na baadaye wamesikiliza mitazamo na miongozo ya Kiongozi Muadhamu kuhusiana na masuala ya wanachuo, vyuo vikuu na majukumu muhimu ya wanafunzi wa vyuo hivyo katika mchakato mzima wa muqawama wa taifa la Iran na masuala mengine tofauti ya leo hii.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kukutana kwake na wanafunzi wa vyuo vikuu tena katika mwezi wa Ramadhani ni jambo linaloupa furaha kubwa moyo wake na kusema kuwa: Masuala ya kila namna pamoja na mitazamo tofuati yaliyotolewa kwenye mkutano huo yalikuwa mazuri na yenye kufurahisha na yanaonesha namna upeo wa kufikikiri na mahitaji ya tabaka la wanachuo ulivyopevuka kama ambavyo yanaonesha kwamba, kadiri muda unavyopita ndivyo misukumo ya kimapinduzi na fikra pana na hoja makini zinavyozidi kuongezeka na kuwa pana zaidi kati ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.
Aidha amewausia wanafunzi wa vyuo vikuu kuzidisha mapenzi yao na kushikamana kwao na Qur'ani Tukufu na dua na kusema kuwa: Nasaha zangu kwa wanachuo ni kujiimarisha kiimani kwani ni kwa kuwa na imani thabiti tu ndipo itawezekana kupata ushindi katika mapambano na jihadi ya kukabiliana na matatizo na mashinikizo ya kila namna.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa hali nyeti na maalumu iliyo nayo Iran hivi sasa inafanana mno na vita vya Ahzab vya kipindi cha Bwana Mtume Muhammad SAW na kuongeza kuwa: Leo hii pia watu wote wanaoabudu dunia na wanaofanya ubeberu duniani wamekusanyana kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wanaushambulia mfumo huu wa Kiislamu kutoka kila upande.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Katika hali kama hii, wale watu ambao wana imani dhaifu na ambao ndani ya nyoyo yao wana mielekeo ya kumpenda adui utawasikia wanatoa maneno ya kuvunja moyo, ya kukatisha tamaa na ya kujiona duni. Lakini watu wenye imani thabiti kadiri hali inavyokuwa nzito na ngumu zaidi, ndivyo wanavyozidi kuwa imara na imani na irada kubwa, na kusimama kidete kukabiliana na hali hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kama tuna nia ya kweli ya kukabiliana na kusimama kidete mbele ya kambi ya kiistikbari na hatimaye kufikia kwenye heshima, hadhi na cheo unachostahiki kuwa nacho mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, tunapaswa kulinda na kutia nguvu taqwa katika matendo yetu kama mtu mmoja mmoja na vile vile katika matendo yetu ya pamoja.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ushahidi kwa kutegemea aya za Qur'ani Tukufu kuhusiana na jinsi vizazi vya baadhi ya qaumu vilivyopotea licha ya vizazi vya kabla yao kuwa ni imani thabiti na kusema: Kuidharau Sala na kufuata matamanio ya nafsi ni mambo mawili makuu yanayomtukumbukiza mja katika kuporomoka kimaadili na kuwa dhaifu katika mapambano.
Ameongeza kuwa: Hiyo ndiyo sababu inayomfanya awasisitizie mara kwa mara viongozi nchini kuhusu kujiepusha kadiri wanavyoweza kufanya pikiniki za kuchanganyika wanafunzi wa kike na kiume, kwani wakati mipaka isipochungwa na hududi za kidini zisipoheshimiwa, matokeo yake huwa ni kujitokeza udhaifu wa imani ndani ya nafsi za watu.
Baada ya kubainisha nafasi ya imani katika suala zima la kusimama kidete na kutotetereka, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia mapambano muhimu mno na asiyoepukika ya taifa la Iran dhidi ya kambi ya kiistikbari na kusema kuwa: Mapambano hayo yalianza pale taifa la Iran lilipoamua kuwa huru na kujitegemea katika kujiletea maendeleo, kwani suala hilo linakinzana kikamilifu na manufaa ya madola ya kibeberu yanayoidhibiti dunia hivi sasa.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, matamshi ya baadhi ya watu wanaodai kuwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unatafuta sababu na kisingizio tu cha kukataa kufikia mapatano na madola ya kibeberu, kwa hakika ni matamshi yasiyoona mbali hata kidogo. Ameongeza kuwa, mapambano haya hayahitajii kisingizio kwa sababu uhakika wa mambo ni kuwa madhali taifa la Iran litaendelea kusimama kidete juu ya msingi wa ghera na kushikamana na Mapinduzi na Uislamu, mapambano hayo ni jambo lisiloepukika, na hayatamalizika ila kwa kutumia mambo mawili, imma Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ijiimarishe vizuri kwa nguvu ilizo nazo na kuulazimisha upande wa pili usithubutu kuichezea, au Jamhuri ya Kiislamu ipoteze utambulisho wake wa asili na ubakie na dhahiri ya juu juu tu isiyo na chochote cha maana ndani yake...