Kiongozi Muadhamu Aonana na Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu na Mabalozi wa nchi za Kiislamu
06/07/2016
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo abubuhi (Jumatano) ameonana na viongozi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu waliopo Tehran na majimui ya wananchi wa matabaka mbali mbali na kusema kuwa, chimbuko kuu la vita, machafuko na ugaidi katika eneo la Mashariki ya Kati na kwenye ulimwengu wa Kiislamu kiujumla ni madola ya kibeberu yanayoongozwa na Marekani. Pia amesisitiza kuwa, lengo na shabaha ya madola hayo ya kibeberu ni kutafuta upenyo wa kuuwezesha utawala wa Kizayuni wa Israel upumue na pia kuisahaulisha kadhia muhimu mno ya Palestina. Ameongeza kuwa: Njia pekee ya kuweza kupambana na kuzishinda njama hizo ni kumtambua vyema adui wa kweli wa Waislamu na kusimama kidete kukabiliana naye. Amesema: Taifa la Iran limethibitisha kivitendo kuwa njia pekee ya kuweza taifa fulani kupata maendeleo, ni istikama na kusimama kwake imara.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa sikukuu ya Idul Fitr na huku akigusia hali uliyo nayo hivi sasa ulimwengu wa Kiislamu na jinsi eneo la Mashariki ya Kati lilivyogubikwa na mauaji, machafuko na miripuko ya umwagaji wa damu amesema: Moja ya mambo muhimu yanayopaswa kufanywa ni kuelewa chimbuko afiriti na khabithi la matatizo ya umma wa Kiislamu leo hii pamoja na mikono ya siri inayoeneza vitendo vya kigaidi duniani.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia namna nchi zote duniani yakiwemo madola ya kibeberu yanayojionesha kidhahiri kuwa yanapinga ugaidi na kufikia hata kuunda muungano wa uongo wa eti kupambana na ugaidi na kusema kwamba: Kinyume kabisa na madai ya kidhahiri na kijuu juu ya madola ya kibeberu, madola hayo kwa kweli ndiyo yanayounga mkono na kueneza ugaidi duniani.
Vile vile amekumbushia namna balozi wa Marekani alivyojumuika na wapinzani wa serikali ya Syria kwenye maandamano yao katika siku za mwanzoni za mgogoro wa nchi hiyo na hivyo kuyageuza malalamiko hayo kuwa mzozo mkubwa wa kisiasa uliopelekea kuzuka vita vya ndani nchini Syria na kusema: Mvutano mdogo wa kisiasa wameugeuza kuwa vita vikubwa vya kuuana ndugu wenyewe kwa wenyewe na hawakuishia hapo, bali wanawasaidia pia kwa silaha na kifedha magaidi pamoja na kuwarahishia kupata mapato haramu ya mafuta, magaidi ambao wameteka maeneo tofauti ya Syria na Iraq na kulitumbukiza eneo la Mashariki ya Kati katika machafuko na matatizo makubwa.
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbushia pia sisitizo lake la mara kwa mara kuhusu sababu za uadui wa Marekani kwa taifa la Iran ambao umekuwa ni uzoefu wa miaka 37 wa kulitambua vyema dola hilo la kibeberu na kuongeza kuwa: Tangu mwanzoni kabisa mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Marekani iliamua kuwa adui wa Imam wetu mtukufu (Imam Khomeini - quddisa sirruh) na harakati yake adhimu na kwamba uadui huo unaendelea hadi leo hii, lakini kutokana na mwamko wa wananchi na kuwa macho Serikali pamoja na kuwa imara viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, njama zote hizo za Marekani zimeshindwa.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, umma wa Kiislamu unapaswa kumtambua vyema adui na kuzielewa vyema njama zake. Ameongeza kuwa: Mfano mwingine wa njama za kuugeuza mvutano mdogo wa kisiasa kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe ni huu unaoshuhudiwa nchini Bahrain hivi sasa.
Amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kuhusika kivyovyote vile katika masuala ya ndani ya Bahrain na katika siku za usoni pia haitajiingiza kwenye masuala hayo, lakini inasema kuwa, kama kuna busara na hekima za kisiasa nchini humo, basi hazipaswi kuruhusu mvutano mdogo wa kisiasa kugeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na si sahihi kuwasukuma wananchi wa nchi hiyo kwenye mapigano ya wao kwa wao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, sababu kuu ya njama zote hizi za mabeberu wa dunia wanaoongozwa na Marekani na ambazo zimeleta maafa makubwa katika eneo hilo, ni kujaribu kulisahaulisha suala la Palestina. Amesema: Mabeberu wanajaribu kukana uwepo wa taifa muhimu katika jiografia ya dunia wakati ambapo Palestina ni taifa lenye historia kongwe ya maelfu ya miaka. Aidha taifa la Palestina ni taifa lenye ardhi yake na haiwezekani kuukana na kuuficha uhakika huo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Utawala wa Kizayuni utapata pigo kutokana na mashinikizo ya kila namna unayoliwekea taifa madhlumu na lililozingirwa kila upande la Palestina.
Ameongeza kuwa: Suala la Palestina ni suala muhimu la ulimwengu wa Kiislamu na hakuna nchi yoyote ya Kiislamu bali hata nchi zisizo za Kiislamu ambayo ina hisia za kibinadamu inayopaswa kuisahau na kuidharau kadhia ya Palestina.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia hali ya nchi Yemen na kuendelea mashambulizi ya kila siku dhidi ya nyumba na makazi ya raia na dhidi ya mahospitali, misikiti na miundombinu ya nchi hiyo na kusisitiza kwamba: Mvamizi wa nchi ya Yemen anapaswa kukomesha mara moja uvamizi wake na ulimwengu wa Kiislamu nao una wajibu wa kumuadhibu mvamizi huyo ambaye ameivamia Yemen kwa sababu za kipuuzi na kufanya mshambulizi makubwa dhidi ya wananchi wa nchi hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia namna taifa la Iran lilivyosimama imara katika kufanikisha masuala yake yote na kusema kuwa: Maendeleo ya Iran ya Kiislamu ni matunda ya kusimama kwake imara na lau kama taifa la Iran lingelisalimu amri mbele ya madola ya kibeberu, bila ya shaka yoyote lisingeliweza kupiga hatua za kimaendelezo lilizopiga leo hii.
Amesema, sababu kuu za kuweza taifa kupata maendeleo ni kusimama imara, ni muqawama, ni kuimarisha muundo wake wa ndani na ni kuwa na azma na nia ya kweli ya kitaifa pamoja na kuwa karibu mno na Mwenyezi Mungu na kuongeza kwamba: Kama taifa fulani litaimarishwa kiimani na kulifanya limtegemee Mwenyezi Mungu tu na kutomuogopa yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, basi bila ya shaka yoyote litafanikiwa katika harakati zake za kuelekea kwenye malengo yake makuu na matukufu.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa maadhimisho ya sikukuu ya Idul Fitr na kusema kuwa, ugaidi, machafuko na idadi kubwa ya wakimbizi ni miongoni mwa matatizo yanayoutesa ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa. Amesisitiza kuwa, kuna wajibu wa kuundwa muungano wa kweli wa kupambana na vitendo vya kigaidi badala ya muungano bandia na wa kimaonyesho na kuongeza akuwa: Kama ilivyofanya huko nyuma, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitosita kutoa mchango wake unaotakiwa katika utatuzi wa matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu na kupambana na njama za maadui zilizoleta maafa makubwa kama ambavyo itaendelea pia kuyaunga mkono na kuyasaidia mataifa yote ya Waislamu bila ya kubagua.
Vile vile Rais Hassan Rouhani amegusia suala la mishahara iliyo kinyume cha sheria na kusema kuwa: Serikali kwa kushirikiana na mihimili mingine mikuu ya dola (Bunge na Mahakama) na kwa uungaji mkono wa wananchi na wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, itaweza kutatua suala hilo na inabidi mbali na kuchukuliwa hatua za haraka, kuweko pia uwazi na kufanyike marekebisho ya sheria na kanuni ili kuzuia kujitokeza tena masuala kama hayo. Amesema, serikali yake itawasilisha muswada maalumu bungeni kwa ajili ya jambo hilo.