Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wananchi wa Matabaka Mbali Mbali
01/08/2016
Shias and Sunnis from different provinces meet with Ayatollah KhameneiAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatatu) ameonana na maelfu ya wananchi wa matabaka mbalimbali kutoka mikoa tofauti ya Iran na kusema kuwa, matatizo ya kimaisha ya watu ni miongoni mwa dhaghadagha na wasiwasi mkubwa uliopo hivi sasa nchini na huku akisisitizia wajibu wa kutegemea uwezo wa ndani ya nchi kama njia pekee ya kutatua matatizo hayo ya wananchi amesema: Makubaiano ya nyuklia ya JCPOA ulikuwa ni uzoefu na umethibitisha kuwa mazungumzo na Wamarekani hayana maana kwani hawana mwamana na kwamba kuna udharura wa kutowaamini maadui katika ahadi zao hasa kwa vile kwa mara nyingine makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yamethibitisha kuwa maadui hasa Marekani si watu wa kuaminika. Ameongeza kuwa, njia pekee ya maendeleo ya nchi na kustawisha hali ya maisha ya wananchi ni kuzingatia uwezo wa ndani ya nchi na si kuwategemea maadui ambao muda wote wanaiwekea vizuizi Iran katika masuala ya eneo la Mashariki ya Kati na duniani kiujumla.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuhudhuria wananchi wa matabaka mbali mbali kutoka mikoa na maeneo tofauti ya nchi kwenye mkutano huo kwamba ni udhibitisho wa jambo hilo kwamba, wananchi wa Iran, pamoja na kuwa na lugha, kaumu na madhehebu na dini tofauti lakini ni wamoja na wameshikamana vilivyo katika kujenga Iran azizi ambayo itakuwa ni mfano bora wa nchi ya Kiislamu na ruwaza na kigezo bora cha kimaanawi na kimaada ulimwenguni, ili kwa njia hiyo mataifa mengine ya Kiislamu nayo yaweze kufuata njia hiyo iliyojaa fakhari na kusimama imara kukabiliana na siasa za kueneza mizozo, fitna, mifarakano na za unyonyonja za mabeberu.
Ameyataja maendeleo makubwa ya kielimu, kisiasa na kijamii ya Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni kitu kinachopaswa kupongezwa kama kutatolewa tathmini ya kiinsafu na ya kiadilifu kuhusiana na jambo hilo. Amesema: Iran ambayo zamani ilikuwa ikitawaliwa na madikteta wa Kipahlavi, ilifanywa tegemezi na iliyobaki nyuma kimaendeleo na dhalili mbele ya Marekani na Uingereza, lakini sasa hivi imekuwa nchi yenye heshima na yenye nguvu ambayo madola ya kibeberu yanaiona ni mpinzani wao mkubwa katika eneo la Mashariki ya Kati na muda wote yanafanya njama za kudhibiti uwezo na suhula zake mbali mbali katika eneo hilo, ingawa tab'an kamwe hawataweza.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ushahidi wa uzoefu wa kihistoria wa kuanzishwa na kunawiri ustaarabu wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Ni jambo lililo wazi kwamba kuifanya Iran kuwa azizi na ruwaza na mfano bora wa nchi ya Kiislamu ni jambo ambalo linahitajia muda wa kutosha na linahitajia juhudi na hima kubwa isiyosita ya viongozi na wananchi, lakini ni jambo linalowezekana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesisitiza kuwa, njia pekee ya kuweza kuifanya Iran kuwa kigezo na mfano wa nchi bora ya Kiislamu, ni kutegemea uwezo na suhula zake za ndani. Ameongeza kuwa: Ili jambo hilo liweze kufanikiwa, kunahitajika kuweko mikakati na mipangilio sahihi, juhudi na bidii isiyosita na kujiweka mbali na uvivu, kuzembea kazi na kuwaamini na kuwategemea maadui.
Ameongeza kuwa: Baadhi ya wakati utamuona adui anaweka vizuizi ambavyo inawezekana kuviondoa kwa kutumia akili na tadibiri, lakini si sahihi hata kidogo kumwamini adui hata kwa sekunde moja.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, uzoefu uliopatikana katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni mfano wa wazi wa usahihi wa udharura wa kutowaamini maadui na kuongeza kuwa: Leo hii hata maafisa wetu wa kidiplomasia na watu waliokuwemo kwenye timu ya mazungumzo hayo wanakariri uhakika huo kwamba Marekani haiheshimu makubaliano hayo na kwamba nyuma ya maneno yao ya upole na ya kupaka paka mafuta, Wamarekani wanaweka vizuizi na wanaharibu uhusiano wa kiuchumi wa Iran nchi nyingine duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kusema: Tab'an ni miaka mingi sasa tumekuwa tukikariri na kurudiarudia suala la wajibu wa kutowaamini Wamarekani, lakini kuna baadhi ya watu ilikuwa ni vigumu kwao kuuamini na kuukubali uhakika huo.
Vile vile amegusia suala la mazungumzo baina ya Iran na kundi la nchi zinazounda kundi la 5+1 barani Ulaya na kusema: Katika kikao hicho, timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran imezikumbusha pande za pili wajibu wao na kuzieleza kuwa hazitekelezi inavyotakiwa makubaliano ya JCPOA na zingalia zinaweka vizuzi katika utekelezaji wa makublaiano hayo.
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbushia namna ilivyopita miezi zaidi ya sita tangu uanze utekelezaji wa makubaliano hayo ya nyuklia na kuhoji kwa kusema: Kwani haikuwa imekubaliwa kwamba vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran viondolewe na athari zake zionekane katika maisha ya watu? Je, baada ya kupita miezi sita tangu makubaliano hayo yafikiwe, kuna athari zozote za wazi zinazoonekana katika maisha ya wananchi? Lau kama Wamarekani wasingelipuuza makubaliano hayo, je, serikali yetu isingeliweza kufanya kazi kubwa na nyingi katika jambo hilo?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ushahidi kutoka katika matamshi ya viongozi nchini waliyoyatoa kabla ya utekelezaji wa makubaliano ya JCPOA na baada ya kuanza utekelezaji wake ya kwamba baada ya Iran kutekeleza ahadi zake, vikwazo vyote vitaondolewa kwa mkupuo mmoja na kusema: Hata hivyo tunachokisikia hivi sasa ni mjadala kuhusu kuondolewa pole pole vikwazo hivyo na sio kuondolewa vyote kwa mara moja. Kwa nini umezuka mjadala huu tena?
Vile vile amegusia namna Wamarekani walivyozungumza kwa maneno laini na mazuri katika barua zao walizozituma kwa viongozi wa Iran na kusema: Karibu miaka miwili iliyopita tulisema kuwa, taifa la Iran linayaangalia mazungumzo hayo ya nyuklia kama uzoefu kwao, ili kuona Wamarekani watafanya nini katika vitendo, na sasa imebainika kuwa, Wamarekani hawaheshimu ahadi zao, na licha ya ahadi mbali mbali walizotoa, lakini bado wanafanya njama na uharibifu dhidi ya Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitizia uzoefu lilioupata taifa la Iran kuhusu vitendo vya Marekani katika kadhia ya makubaliano ya JCPOA na kusema: Wamarekani wanatwambia njooni tufanye mazungumzo katika masuala ya eneo la Mashariki ya Kati, lakini uzoefu uliopatikana kwenye JCPOA unatwambia kuwa, jambo hilo ni sumu kali mno, na kwamba haiwezekani kuyaamini maneno ya Wamrekani katika jambo lolote lile.
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kama adui wa mtu fulani atakuwa anaheshimu angalau maneno yake, inawezekana kufanya mazungumzo na adui huyo katika baadhi ya mambo, lakini kama adui atafanya kama wanavyofanya Wamarekani kutoheshimu hata maneno yake, na tofauti na tabasamu anazotoa hadharani, akawa hajali hata kidogo kwenda kinyume na ahadi zake, haiwezekani na haipasi kufanya mazungumzo na adui wa namna hiyo na uhakika huo ndiyo sababu ya mimi kukataa mara kwa mara kufanya mazungumzo na Wamarekani.
Amesema, matatizo na changamoto za eneo la Mashariki ya Kati haziwezi kutatuliwa kwa mazungumzo baina ya Iran na Marekani na kusisitiza kuwa, inabidi kufanyike juhudi za kweli na zinazofuata njia sahihi za kuleta ustawi wa kimaada na kimaanawi nchini, wakati huo ndipo zote tutakapomuona adui akitukimbilia akijaribu kuwa karibu nasi kutafuta urafiki na si kutufanyia uadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ushahidi kutoka katika matamshi ya maafisa wa kidiplomasia wa Iran na kusema: Wamarekani wanataka wachukue wao kila kitu na wasitoe chochote na kwamba kufanya mazungumzo na dola kama hilo kuna maana ya kwenda kinyume na njia sahihi ya maendeleo yetu nchini, kama ambavyo kuna maana ya kulegeza misimamo mtawalia mbele ya dola hilo na kukubali kubeba kivitendo ubeberu wake pamoja na ukosefu wake wa uaminifu na kutoheshimu kwake ahadi linazotoa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia matamshi yenye maana pana sana ya Imam Khomeini (Ridhwanullahi Ta'ala Alayh) kwamba Marekani ni shetani mkubwa na kuongeza kuwa: Kwa mujibu wa aya za Qur'ani Tukufu, Siku ya Kiyama, shetani atawaambia wafuasi wake kwamba wajilaumu wao wenyewe kwa sababu waliamini ahadi zake za uongo, leo hii pia wajibu uliopo ni kutozingatia uongo wa ahadi za Marekani na kutomwamini shetani huyo mkubwa, na huo ni udhibitisho wa kivitendo wa suala hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei amewataka vijana na watu wenye vipaji wa Iran kuzingatia vizuri siasa zinazoendelea nchini kuhusiana na Marekani na kuongeza kuwa: Siasa hizo zimeundika juu ya msingi wa uzoefu, kumuelewa adui na kuelewa uhakika na hali halisi ilivyo nchini; ilivyo katika eneo na ilivyo duniani leo hii.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema katika sehemu nyingine ya hotuba yake kwamba kuna wajibu kwa viongozi wa Iran kutegemea kinadharia na kivitendo uwezo mwingi na vipaji vya kila namna vya ndani ya nchi, kuhuisha taasisi ndogo ndogo na za kati na kati na kuupa umuhimu uchumi unaotegemea elimu za kimsingi ili kwa njia hiyo waweze kupunguza vyema matatizo yaliyopo.
Vile vile amewataka wananchi kutilia hima mno suala la kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi zikiwemo bidhaa za vifaa vya nyumbani na kuongeza kuwa: Licha ya kusisitiziwa mno udharura wa kupigwa marufuku kuingiza nchini bidhaa ajinabi ambazo mithili yake zinazalishwa humu nchini, lakini masoko ya Iran yamejaa bidhaa za kigeni, jambo ambalo linaiweka chini ya mashinikizo sekta ya ndani ya nchi ya uzalishaji wa bidhaa hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, ni jambo la dharura kikamilifu kupambana vilivyo na wafanya magendo wakuu na kuteketeza kikamilifu bidhaa za magendo na kuongeza kuwa, kama hali itaendelea hivi hivi ilivyo leo, maana yake ni kuwakosesha kazi vijana wetu, kuzidi kuzorota uchumi na maisha ya wananchi kuwa magumu na kwa hakika mambo hayo si ya kutatuliwa kwa kuwa na uhusiano na Marekani au Ulaya, bali ni kwa viongozi kuchukua hatua za kivitendo za kufanikisha jambo hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amesema, matatizo ya kimaisha ya wananchi ndiyo daghadagha na wasiwasi wa kila siku uliopo nchini na kuongeza kuwa: Ushauri wote uliotolewa na wanafikra tofauti unaonesha kuwa, njia pekee ya kuweza kutatua matatizo hayo ni kuzingatia uwezo wa ndani ya nchi.
Amesema, ziara zilizofanywa nchini na wafanya biashara wa kigeni kwa uchache hadi sasa hazijazaa matunda na kuongeza kuwa: Lengo la wafanya biashara hao ni kuhodhi soko la ndani ya Iran la matumizi, wakati ambapo safari za namna hiyo zinapaswa ziishie kwenye uwekezaji wa kweli na kuhamishia nchini teknolojia na sio kuingiza bidhaa za kigeni kwa ajili ya matumizi tu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kupambana na ufisadi kuwa ni katika masuala muhimu mno na kuongeza kuwa: Alhamdulillah, viongozi nchini wametangaza waziwazi kuwa, watapambana vilivyo na mishahara mikubwa kupindukia na watu wanaokomba mali za umma na tayari kumeshachukulia hatua katika baadhi ya sekta, suala ambalo linapaswa liendelee kwa wigo mpana zaidi.
Vile vile amewataka viongozi nchini Iran kupambana na maisha ya anasa kwa maneno na kwa vitendo na kuongeza kuwa: Wakati maisha ya anasa yanapokita mizizi katika jamii, maporomoko ya madhara yake yanaishia kwa watu wa kawaida, hivyo kuna wajibu wa kupambana kikamilifu na utamaduni wa maisha ya anasa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria lengo la mwaka huu wa Kiirani wa 1395 Hijria Shamsia la kuitwa mwaka wa Uchumi wa Kimuqawama, Hatua na Vitendo na kuongeza kusema: Tab'an kuna kazi zimefanyika hadi hivi sasa kufanikisha uchumi huo, lakini inabidi wananchi wahisi na waone matunda ya kazi hizo katika maisha yao ya kila siku.
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia suala la hali iliyojaa makelele leo hii katika eneo la Mashariki ya Kati, na huku akitoa tathmini jumla kuhusu suala hilo amesema: Marekani inahusika pia katika hata masuala hayo.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kutangazwa hadharani uhusiano uliopo baina ya serikali ya Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni sawa na kuupiga jambia kwa nyuma umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Hatua hiyo ya Wasaudia ni dhambi na usaliti mkubwa, lakini Wamarekani wanahusika kwenye ghalati na kosa hilo kubwa kwani serikai ya Saudi Arabia ni mfuataji tu na imedhibitiwa na Marekani bali ni mtekelezaji wa kila amri inayotoka kwa serikali ya Marekani.
Amesema, kuvamiwa Yemen na kushambuliwa kwa mabomu mfululizo nyumba za raia, mahospitali na mashule na kuendelea kuuliwa kila siku watoto wadogo nchini humo ni uhalifu mwingine mkubwa unaoendelea kufanywa na serikali ya Saudi Arabia na kuongeza kuwa: Jinai hizo nazo zinafanyika kwa kutumia silaha za Marekani na kwa baraka kamili za dola hilo la kibeberu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa, hata wakati Umoja wa Mataifa ulipotia nia ya kulaani jinai hizo tena baada ya kupita muda mrefu wa kukaa kimya, mdomo wa Umoja wa Mataifa ulifungwa kwa hongo ya fedha, vitisho na mashinikizo.
Ameongeza kuwa: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwenye utendaji mbovu alikiri kuwekewa mashinikizo hayo, lakini badala ya kukaa na kukiri kwa maneno tu, ilimpasa ajiuzulu cheo hicho na sio kuendelea kushikilia cheo hicho na kuusaliti ubinadamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la Bahrain na kumiminwa jeshi la kigeni nchini humo kwa ajili ya kuwaweka chini ya mashinikizo wananchi wa nchi hiyo kuwa ni mfano mwingine wa vitendo vinavyoungwa mkono na Marekani na kusisitiza kuwa: Leo hii serikali ya Saudia inaongozwa na watu wanagenzi lakini uchanganuzi wa kina wa masuala hayo unaonesha kuwa, mambo yote hayo yanafanywa na Marekani.
Vile vile amegusia nafasi ya Wamarekani katika kuanzisha na kuyatia nguvu makundi ya kitakfiri kwa shabaha ya kuzusha mifarakano katika umma wa Kiislamu na kueneza Uislamu wa Kiummawi na Kimarwan sambamba na kuchafua jina la Uislamu sahihi na halisi na kuongeza kuwa: Wamarekani wanadai kuwa, eti wanapambana na makundi ya kitakfiri na wameunda muungano wa kupambana na makundi hayo wakati ambapo muungano huo haujafanya lolote la maana bali kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, muungano huo hata unayasaidia makundi hayo katika baadhi ya mambo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema: Tab'an makundi hayo ya kitakfiri leo hii yanawadhuru hata hao walioyaanzisha na kuyaunga mkono na hilo ni kama sisi Wairani tunavyosema, ‘apandaye upepo, huvuna kimbunga.'
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa muhtasari wa namna fulani wa hotuba yake kwa kusema kuwa, Marekani ndiyo iliyozusha na kushadidisha matatizo katika eneo la Mashariki ya Kati na kusisitiza kuwa: Mataifa ya eneo hili yanao uwezo wa kutatua masuala yao hayo bila ya kuhitajia msaada wa madola ya kigeni na sisi sambamba na kutoa mwito kwa tawala za nchi za eneo hili, tunapenda kuzikumbusha kuwa Marekani haiaminiki na inaziangalia tawala za nchi za Kiarabu kwa jicho la nyenzo tu za kuimarisha uwepo wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kufanikishia malengo yao ya kibeberu.
Amesema, utatuzi wa matatizo ya Mashariki ya Kati ni kuungana mataifa na tawala za nchi za Waislamu pamoja na kusimama imara kukabiliana na malengo ya kibeberu ya Marekani na baadhi ya madola ya Ulaya na kuongeza kuwa: Inabidi kuyaelewa vizuri malengo hayo na kusimama imara kukabiliana nayo kama ambavyo taifa letu limesimama imara kwenye njia hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Pamoja na kuweko njama zote hizo za Wamarekani, lakini njama na mipango yao imefichuka na kadiri siku zinavyopita, ndivyo Marekani inavyozidi kuwa dhaifu katika eneo la Mashariki ya Kati.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, uingiliaji na uadui wa Marekani hauishii tu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: Katika matukio ya hivi karibuni ya nchini Uturuki, kuna tuhuma kali kwamba jaribio hilo la mapinduzi ya kijeshi limepangwa na kuendeshwa na Wamarekani na kama hilo litathibitika, itakuwa ni kashfa kubwa kwa Marekani.
Vile vile ameashiria uhusiano mkubwa wa Uturuki na Marekani ambapo Uturuki inahesabiwa kuwa ni muitifaki wa kieneo wa Marekani na kusema kuwa: Wamarekani wanapinga Uislamu na fikra za Kiislamu hivyo wameamua kufanya mapinduzi ya kijeshi hata nchini Uturuki kutokana na kuweko huko mielekeo ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwa kusema: Tab'an harakati hiyo ya ukandamizaji imepelekea Marekani kuchukiwa na wananchi wa Uturuki, huku hali ya Wamarekani ikizidi kuwa dhaifu mbele ya wananchi wa nchi za Iraq, Syria na maeneo mengine duniani.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia ahadi za Mwenyezi Mungu zisizo na shaka kutimia kwake za kuwanusuru wanaoinusuru dini Yake na kusema: Kama taifa la Iran litakuwa na nia na itikadi ya kweli kuhusiana na ahadi hiyo ya Mwenyezi Mungu na kuandaa mazingira ya kutimia kwake, basi matatizo yake yote yataondoka.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia kukaribia mwezi wa (Mfunguo Pili) Dhilqaad ambao ni moja ya miezi minne mitukufu na kusema: Kuitwa miezi hiyo kwa jina hilo kuna maana ya kuwa Mwenyezi Mungu ameipa heshima kubwa zaidi miezi hiyo kiasi kwamba ni haramu kufanya baadhi ya mambo kwenye miezi hiyo na ni kutokana na heshima hiyo iliyotolewa na Mwenyezi Mungu kwa miezi hiyo ndio maana tunapaswa kujikurubisha zaidi kwa Mwenyezi Mungu ndani ya miezi hiyo mitukufu kwa ajili ya kujiimarisha zaidi kimaanawi.
Mkutano huo umehudhuriwa na watu wa matabaka mbali mbali kutoka mikoa ya Azerbaijan Magharibi, Ardebil, Sistan na Baluchistan, Lorestan, Kerman na Kermanshah.