Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Maimamu wa Misikiti ya Mkoa wa Tehran
21/08/2016
Ayatollah Khamenei met with Prayer Leaders from across Tehran provinceAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Jumapili) ameonana na maimamu wa misikiti na wa Sala za jamaa wa mkoa wa Tehran na kusema kuwa, msikiti ni kituo muhimu cha kukusanyika watu, kufanya mashauriano, kuimarisha muqawama na kuweka mipango muhimu pamoja na kufanya harakati za kijamii na kiutamaduni. Aidha ameashiria udharura wa kuimarishwa imani ya kidini kati ya watu ikiwa ndiyo nguzo kuu ya Mapinduzi ya Kiislamu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: Kuna wajibu wa kuuchambua na kuupa muelekeo sahihi mchakato jumla wa harakati ya jamii kuhusu masuala yanayoendelea kwa kuangalia pande zote za masuala hayo na kwa mtazamo wa kiutamaduni kama njia ya kumuainishia majukumu kila mtu katika jamii.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbushia falsafa ya kuainishwa Siku ya Kimataifa ya Msikiti na kuongeza kuwa: Siku hii ambayo kimsingi ni siku ya kimapinduzi, ilipasishwa na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC kwa mashinikizo na maombi ya Jamhuri ya Kiislamu na kutokana na Wazayuni kuuchoma moto Msikiti wa al Alqsa na kwa lengo la kuufanya umma wa Kiislamu usimame imara kukabiliana na utawala wa Kizayuni; hivyo kuna wajibu wa kuzingatiwa siku hiyo kwa kutilia maanani mambo hayo.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesema, suala la msikiti ni ubunifu wa dini tukufu ya Kiislamu kwa ajili ya kuipa muundo maalumu jamii na kuwa na mawasiliano na watu katika mhimili wa dhikr, sala na kumzingatia Mwenyezi Mungu. Ameongeza kuwa: Katika historia ya Uislamu, misikiti ilikuwa ni kituo kikuu cha mashauriano, ushirikiano na kuchukua maamuzi kuhusu masuala muhimu ya kijamii, kisiasa na kijeshi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia pia umuhimu wa kuzingatiwa Sala na kuongeza kuwa: Ibada ya Sala inabidi itekelezwe kwa njia bora kabisa na kwa kumzingatia vilivyo Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwa kujiweka mbali maradhi kama mghafala, riya na kujionesha kwa watu. Amesema, maimamu wa misikiti wana jukumu zito na kubwa la kubainisha na kueneza kielimu na kwa ulimi umuhimu wa Sala ambayo ni uhakika mwenye mvuto na shauku.
Amesema: Msikiti ni kituo kikuu cha kazi zote za kheri na kuongeza kuwa: Msikiti unapaswa kuwa kituo kikuu cha kuwajenga watu, kuimarisha nyoyo na kuongoza vizuri mambo ya kidunia, kukabiliana na adui, kuongeza kiwango cha busuri na muono wa mbali na sehemu ya kuandalia mazingira ya kuundika ustaarabu wa Kiislamu. Hivyo jukumu la imamu wa msikiti mbali na kusalisha jamaa, apiganie kusimamishwa haki na uadilifu, kufundisha na kubainisha masuala ya dini pamoja na kuielimisha jamii hukumu za dini ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, imamu wa jamaa ndiye mhimili wa msikiti na kuongeza kuwa: Uimamu wa msikiti ni kazi muhimu na ya kimsingi na si sahihi kuliangalia kijuu juu tu jukumu hilo muhimu, wala kudharauliwa haki na heshima ya msikiti, bali inabidi imamu awepo msikitini muda wote na awasalishe Waislamu kwa kutekeleze kwa njia bora kabisa ibada ya Sala, akae kusikiliza mahitaji ya watu, aweke darsa mbali mbali za kufundisha dini pamoja na kujibu maswali hasa ya vijana; na ni kwa njia hiyo ndipo atakuwa ameutendea haki yake msikiti.
Amesema, kuweza kuugeuza msikiti kuwa mhimili na marejeo makuu ya mambo yote kuwa ni katika vipaji vikubwa vya Imam Khomeini (quddisa sirruhu) alivyovionesha katika siku za awali kabisa za Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Msikiti ni kituo kikuu cha kazi za aina zote za kijamii na kwamba msikiti una mchango mkubwa sana katika kutia nguvu fikra na kuwahamasisha watu kufanya mambo mbali mbali mazuri ya kijamii.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja misikiti kuwa ndio msingi mkuu wa muqawama hususan muqawama wa kiutamaduni na kusisitiza kuwa: Kama kutakosekana ngao madhubuti ya kulinda utamaduni, basi mambo yote yatapotea.
Vile vile amezitaja njama tata na za kila namna za maadui za kujaribu kujipenyeza katika masuala ya kiutamaduni nchini Iran ni kubwa mno hivi sasa ikilinganishwa na hali ilivyokuwa awali ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Shabaha kuu ya njama hizo za mtawalia na zenye matabaka kadhaa ni imani ya kidini ya wananchi wa Iran, ambao ndio nguzo kuu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na ndio waliofanikisha kuundwa Jamhuri ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameyataja Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni zilizala kubwa iliyozikumbwa nguzo za mfumo wa kibeberu duniani na kuongeza kuwa: Kwa baraka za "Uislamu wa Kimapinduzi" na "Mapinduzi ya Kiislamu" lengo kuu la mabeberu wa dunia yaani kulidhibiti eneo la Mashariki ya Kati limeshindwa na kwamba Marekani hivi sasa imekwama vibaya katika eneo la magharibi mwa Asia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ameongeza kuwa: Lau kama taifa la Iran lisingelikuwa limeshikamana vilivyo na imani, Iran nayo ingelikuwa mithili ya nchi nyingine zilizoko chini ya mwavuli wa Marekani na madola mengine yasiyo Marekani na ni kwa sababu hiyo ndio maana maadui hao wakawa na chuki kubwa sana na zisizo na kikomo dhidi ya imani ya wananchi wa Iran.
Amesema, vijana ndio shabaha kuu ya maadui wanaofanya njama za kujipenyeza katika masuala ya kiutamaduni kwa lengo la kudhoofisha imani na itikadi za wananchi wa Iran na kuongeza kwamba: Licha ya kuweko njama zote hizo za upotoshaji, lakini leo hii kuwepo wimbi kubwa la vijana wenye imani thabiti wa Iran kunazidi kuonesha muujiza mkubwa wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwamba vijana wa leo hii wana hamasa na wako mstari wa mbele zaidi ikilinganishwa na vijana wa kipindi cha awali ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja nafasi ya misikiti katika kuongeza muqawama na kuimarisha ngao ya kiutamaduni kuwa ni jambo muhimu na kuongeza kwamba: Msikiti ni kituo kikubwa cha kazi za kujitolea na kufanyia harakati za kiutamaduni.
Vile vile amesema, maimamu wa misikiti wanapaswa kutumia kadiri wanavyoweza mbinu sahihi na bora misikitini na wawe ni kigezo kizuri kwa wengine. Amesisitiza kuwa: Kuweka vikao vya moja kwa moja na wananchi ni mbinu nyingine za tablighi na yenye taathira kubwa katika vyombo mbali mbali.
Aidha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha nukta nyingine muhimu kwa kusema kuwa, utamatuni na kuwa na busuri na muono wa mbali kiutamaduni ndio msingi sahihi wa kuendeshea siasa na kusisitiza kuwa: Siasa katika maana yake ya halisi, si kuwa mfuasi wa huyu au yule, bali maana yake ni kuwa na mtazamo mpana kuhusu mambo mbali mbali na kuwa na uwezo wa kuichanganua inavyopasa harakati kuu ya jamii.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kwa mtazamo wa siasa sahihi, kuna wajibu wa kuchunguza harakati kuu ya jamii na kujibu maswali kadhaa ya kimsingi na yaliyo wazi ambayo ni kujiuliza je, mtindo wa maisha yetu leo hii unatupeleka wapi? Je, tunaelekea upande wa uadilifu wa kijamii, uhuru wa kweli na kuundika ustaarabu wa Kiislamu au mtindo huo unatusukuma upande wa kuwa tegemezi kwa Marekani na kuathiriwa na muundo na mambo yanayofanyika katika nchi za Magharibi?
Ameendelea na hotuba yake kwa kusema: Tab'an, kwa kuwa na mtazamo huo jumla na utafiti wa kina kuhusiana na uhalisia wa mambo, kunabainisha hatima ya masuala yanayoendelea na maamuzi anayopasa mtu kuchukua kuhusiana na watu, vyama na makundi mbali mbali ya kisiasa.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa mfano wa kufafanua zaidi matamshi yake kuhusiana na umuhimu wa kuwa na mtazamo na uchanganuzi mkubwa na sahihi wa mambo kwa kusema: Awali ya fitna (iliyotokea mwaka 2009 mjini Tehran), nilimwambia mmoja wa viongozi wa fitna hiyo kwamba wewe kijuu juu unaonekana ni mfuasi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kwa maneno yako mwenyewe ni kwamba unachopinga wewe ni matokeo ya uchaguzi tu, lakini unapaswa kutambua kuwa uongozi wa mambo haya mnayoyafanya utachukuliwa na mabeberu ambao watatumia vitendo vyenu hivi kuulenga mfumo wenyewe wa Jamhuri ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Watu hao - tab'an kama tutaviangalia kwa jicho zuri vitendo vyao - hawakufahamu maneno yangu na waliingia kwenye fitna hiyo na kila mmoja aliona mwenyewe namna matokeo ya uchaguzi yalivyotumiwa kama kisingizio cha kuushambulia na kuupinga mfumo mzima wa Jamhuri ya Kiislamu.
Vile vile amesema: Kuna baadhi ya watu wanasema kuwa, yaliyotokea wakati huo yameshapita, tuachane nayo, lakini kuna wajibu wa kuzingatia kuwa kama kutatolewa maneno yaliyo kinyume na msimamo wa mtu anayedaiwa kufuatwa na kuungwa mkono na watu fulani, wajibu wa mtu huyo ni kujitokeza na kupinga matamshi hayo, vinginevyo maneno hayo yatahesabiwa kuwa ndio msimamo wake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendeleza hotuba yake mbele ya maimamu wa misikiti ya mkoa wa Tehran kwa kugusia nukta nyingine kadhaa muhimu.
Kusimamisha Sala za jamaa nyakati zote za Sala, na kuhakikisha kuwa misikiti inakuwa wazi kwa ajili ya kupokea watu na kusali katika muda wowote ule wa siku, ni miongoni mwa nukta hizo zilizogusiwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake hiyo.
Vile vile amekosoa mtazamo unaonesha kuwa misikiti ni kwa ajili ya kusali tu na kusema: Fikra hiyo mgando kwa hakika ndio huo usekulari ambao unaihesabu dini kuwa inaishia katika matendo ya mtu binafsi tu na kuzuia kuingia dini katika masuala ya kijamii na kisiasa.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi zaidi kwa kusema: Uislamu wa kisekulari na unaofungwa tu katika utekelezaji wa ibada ziwe za mtu binafsi au za kijamii, hata ukitokezea kuwa na wafuasi wengi namna gani, hauwezi kufanyiwa uadui na mabeberu bali kitu ambacho kinafanyiwa uadui na waistikbari wa dunia ni Uislamu wenye nguvu ambao unaunda mfumo wa kisiasa na kijamii na kuwaongoza watu kuelekea kwenye ufanisi na mafanikio ya kweli ya duniani na Akhera.
Kuwapa mazingatio maalumu vijana na kuthamini nafasi maalumu ya kizazi cha vijana ni nukta nyingine ambayo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewausia maimamu wa misikiti ya mkoa wa Tehran.
Amewaambia maimamu hao kwamba: Fanyeni juhudi za kuzivutia nyoyo za vijana ili zipende kushiriki vilivyo katika masuala ya misikiti kwa kutumia vivutio mbali mbali na sahihi yaani kwa matamshi na hatua zilizochanganyika na umaanawi na irfani ya kweli ili kwa njia hiyo nchi ya Iran na jamii yake iweze kufaidika vizuri na mahudhurio makubwa ya vijana misikitini.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amehimiza kuhusu wajibu wa kuhifadhiwa historia ya misikiti kwa njia tofauti kama vitabu, picha n.k kwa ajili ya kuwaelimisha vijana wa leo na wa kesho kuhusu nyumba hizo za Mwenyezi Mungu.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Licha ya kuweko uadui mkubwa na ulio tata sana wa madola ya madhalimu ya kibeberu tena kwa siri na kwa dhahiri, lakini neno jema la Jamhuri ya Kiislamu linazidi kupata nguvu na kuimarika siku baada ya siku, na kwa baraka za imani ya kweli na mshikamano wa wananchi, njama zote hizo zitaendelea kushindwa.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Alhaj Ali Akbari, mkuu wa kituo cha huduma za misikiti nchini Iran ametoa ripoti fupi kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Msikiti na kusema kuwa: Msikiti ni sehemu ya kuandaa mazingira ya kuongeza busuri na muono wa mbali wa watu na ni kituo cha kulea wanajihadi na waumini wa kweli wenye hadhi ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Alhaj Ali Akbari aidha amesema, zaidi ya asilimia 97 ya mashahidi wa Iran ni watu waliopata malezi misikitini na kuongeza kuwa: Kuainisha malengo, kujenga utamaduni wa kupenda misikiti, ushirikiano baina ya maimamu wa misikiti, kuundwa kambi ya pamoja na iliyoshikamana na kujenga utamaduni, kutumia uwezo wa watu wenye vipaji na vijana, kuongoza misikiti kwa kuwashirikisha wananchi na kutumia uwezo wa misikiti kwa ajili ya kujenga jamii ya waumini wa kweli ni katika malengo makuu na mipango ya misikiti nchini Iran.