Ujumbe wa Shukrani kwa Msafara wa Wanamichezo wa Iran katika Olimpiki ya Rio 2016
23/08/2016
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe maalumu wa maandishi wa kuwashukuru wanamichezo nguli na bingwa waliotwaa medali pamoja na wanamichezo wote wengine na makocha wao wanaofanya jitihadi kubwa za kuimarisha sekta ya michezo nchini, waliokuwemo kwenye msafara wa wanamichezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mashindano ya Olimpiki ya mwaka huu wa 2016 yaliyofanyika Rio de Janeiro, Brazil.

Matini kamili ya ujumbe huo ni kama ifuatavyo:

 

Kwa jina Lake Mtukufu
Ninatumia fursa hii kuushukuru msafara wa wanamichezo wetu uliorejea nchini kutoka katika mashindano ya Olimpiki. Ninawashukuru wanamichezo bingwa waliotwaa medali na kuzifurahisha nyoyo za wananchi wenzao, na pia mabingwa waungwana ambao walinyimwa haki yao kutokana na uamuzi mbovu wa waamuzi na pia kwa wanamichezo ambao kushindwa kwao kupata mafanikio kwenye michezo hiyo hakuwapunguzii chochote katika thamani ya juhudi zao kubwa. Shukrani zangu ziwaendee pia akinamama wanamichezo ambao wamewaonesha walimwengu kwa sura ya kujivunia - vazi la Kiirani na kwa mwanamama shujaa ambaye aling'ara na vazi lake la Hijabu wakati akiongoza msafara wa Iran kwenye michezo hiyo, kama ambavyo ninawashukuru pia makocha na wanamichezo wa siku nyingi wa Iran. Nasema karibuni nchini kwenu. Tunajua thamani yenu.

Sayyid Ali Khamenei
2 Mwezi Shahrivar 1395
(Agosti 23, 2016)


Itakumbukwa kuwa, msafara wa wanamichezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umerejea nyumbani ukiwa umeshinda medali tatu za dhahabu, moja ya fedha na nne za shaba na kushika nafasi ya ishirini na tano katika mashindano ya Olimpiki ya Rio 2016.