Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Familia ya Shahid Rajab Mohammad Zadeh
28/08/2016
Familia ya shahid Alhajj Rajab Mohammad Zadeh, leo asubuhi (Jumapili) imeonana na Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mazingira yaliyojaa mapenzi na kushibana.
Katika mazungumzo hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameienzi hadhi na cheo cha kimaanawi alichokuwa nacho shahid Mohammad Zadeh na kusema kuwa, katika kipindi cha miaka yote hii, shahidi huyo majeruhi wa vita alivumilia maumivu makubwa kutokana na majeraha aliyokuwa nayo, lakini kila sekunde na kila saa aliyovumilia, atapata ujira bora mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambapo hatimaye mja huyo mwema amefuzu kwa kufa shahidi na hivyo kuzidi kupanda daraja za juu za kimaanawi mbele ya Mola Muumba.
Ayatullah Udhma Khamenei ameienzi na kuipongeza pia roho na moyo wa hali ya juu wa kujitolea na subira wa familia ya shahid Mohammad Zadeh hususan mke wa shahid huyo na kuongeza kwa kuwaambia: Nyinyi familia za mashahidi ni dhihirisho na nguzo ya Mapinduzi ya Kiislamu, nasi huwa tunapata moyo mkubwa zaidi kila tunapoonana nanyi wapendwa.
Vile vile amehimiza kupewa umuhimu suala la kubainishwa na kutangazwa sira na maisha mazito lakini yenye fakhari kubwa ya mashahidi kama shahid Mohammad Zadeh.
Alhaj Rajab Mohammad Zadeh ambaye asilimia 70 ya mwili wake ulipata ulemavu baada ya kujeruhiwa katika vita vya kujihami kutakatifu (vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa Saddam dhidi ya dola changa wakati huo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) alijeruhiwa vibaya baada ya kugongwa na roketi kichwani na kwenye uso na kupata daraja ya kuwa majeruhi wa vita hivyo vitakatifu.