Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Maafisa wa Kamati ya Sensa ya Watu
13/09/2016
8th National Population and Housing CensusAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumanne) ameonana na maafisa wa Kamati ya Sensa ya Watu na Makazi na wajumbe wa Baraza Kuu la Takwimu la Iran pamoja na wakurugenzi wa Kituo cha Takwimu cha Iran na kusisitiza kwamba, suala la kuwa na takwimu na taarifa za kina zilizokusanywa kiutaalamu na kukusanywa sehemu moja ndio msingi mkuu wa maamuzi sahihi na ya kina kwa nchi. Vile vile amesisitizia umuhimu wa kufanyika sensa ya watu wote na amewaambia wananchi kwamba: Wananchi wote azizi wanapaswa kulipa uzito mkubwa zoezi hili muhimu na kushiriki vilivyo kulifanikisha.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, takwimu ni jambo lenye udharura wa kipekee na ni muhimu mno kwa ajili ya kuweka mipango kuhusu vyanzo na mahitaji ya kila aina na mengi ya nchi na kuongeza kuwa: Wananchi azizi wa matabaka mbali mbali ya wananchi wanapaswa kushiriki vilivyo katika zoezi hilo kwa ajili ya kuiwezesha nchi yao kuchukua maamuzi sahihi, yanayofaa na ya wakati mwafaka na vile vile wana wajibu wa kuzipa taasisi za takwimu taarifa na maelezo sahihi na wanapaswa wajue kuwa, kama walivyosisitiza viongozi nchini, takwimu zinazotolewa zitaendelea kuwa siri.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na nasaha zake kwa kuwaeleza wahusika wa masuala ya takwimu nchini Iran akiwaambia: Katika ukusanyaji wa takwimu inabidi hali iliyopo ibainishwe na kasi ya ymabadiliko nao ujulikane kwani mabadiliko yanayotokea hivi sasa yanatokea kwa kasi kubwa, hivyo viongozi na wachukuaji maamuzi ya nchi wanapaswa wawe na takwimu za uhakika na za kina ili wasije wakabakia nyuma mbele ya kasi hiyo ya mabadiliko.
Amesema, inasikitisha kuona kuwa, nchi yetu iko nyuma katika upande wa kukusanya takwimu kiasi kwamba hata kuna baadhi ya maeneo, viongozi hawana takwimu za uhakika kuhusiana na sekta hizo.
Ametoa mfano wa umuhimu wa kukusanya takwimu kwa kusema: Uchumi unaotegemea taasisi na mashirika ya elimu za kimsingi ndiyo njia bora ya maendeleo ya nchi kwani unategemea nguvu kazi ya watu wasomi na wabunifu, sasa inabidi ijulikane wazi katika kila sekta ya uchumi na utaalamu, kuna vijana wangapi na wataalamu kiasi gani wenye uwezo wa kutekeleza ipasavyo kazi wanazotakiwa kwa kutumia vizuri vipaji na ubunifu wao.
Amesema, utatuzi pekee wa matatizo ya nchi ni uchumi wa kimuqawama kwani kwa kuwepo uchumi huo na hata ikawa njia zote zimefungwa duniani, nchi haiwezi kupata matatizo kwani itakuwa inategemea uchumi wake wa kujitegemea ndani lakini kama uchumi hautakuwa wa kutegemea vyanzo vya ndani ya nchi, hatima ya uchumi huo ni kuporomoka...