Kiongozi Muadhamu Aonana na Wananchi wa Matabaka Mbali Mbali kwa Mnasaba wa Idul Ghadir
20/09/2016
Eid al GhadirSambamba na maadhimisho ya sikukuu ya Ghadir, idi ya Uimamu na Wilaya, na sikukuu ya Allahu Akbar, leo asubuhi (Jumanne), Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei ameonana na maelfu ya wananchi wa matabaka tofauti katika Husainia ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) mjini Tehran.
Katika mkutano huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa sikukuu ya Ghadir na kusema kuwa, ujumbe muhimu zaidi unaopatikana katika tukio la Ghadir ni kuainishwa Uimamu kuwa ndio msingi na kielelelezo cha utawala katika Uislamu. Aidha amegusia sifa za kipekee za Imam Ali (Alayhis Salaam) hususan namna alivyokuwa ametimiza sifa zote za kuongoza dola ya Kiislamu, na amewausia hadhirina kuhusu ulazima wa kushikamana na Wilaya na utawala wa Amirul Muminin, Imam Ali (Alayhis Salaam) kupitia kutekeleza vizuri miongozo na nasaha za shakhsia huyo mkubwa na wa aina yake.
Vile vile amegusia baadhi ya maneno yanayotumika kuitambulisha sikukuu ya Ghadir kama vile kuiita idi kubwa ya Mwenyezi Mungu na kusema kuwa, sababu ya kuweko majina hayo, ni tukio muhimu sana ambalo lilitokea katika Ghadir, nalo ni kuainishwa kigezo na kielelezo cha utawala ndani ya dola ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Kielelezo na kigezo hicho ni Uimamu na Wilaya katika jamii ya Kiislamu na ambayo ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu iliyotangazwa na Bwana Mtume Muhammad SAW.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Mbali na kuainisha kigezo na kielelezo, Imam Ali (Alayhis Salaam) alitangazwa rasmi kuwa ni Imam akiwa ni shakhsia mkubwa, mtukufu, aliyejaa nuru na ambaye si rahisi kumtia doa.
Ameongeza kuwa: Tab'an, hakuna mtu yeyote aliyeweza kufikia kilele alichofikia Imam Ali AS katika upande wa Uimamu na kuongoza jamii ya Kiislamu baada ya Bwana Mtume SAW. Shakhsia wengine wakubwa wa kielimu na uchaji Mungu wamekuja katika historia ya Uislamu, kama vile Imam wetu mtukufu (Imam Khomeini - quddisa sirruh), lakini wote hao ni tone tu mbele ya miale iliyojaa nuru ya Amirul Muminin Imam Ali (Alayhis Salaam).
Baada ya hapo ametoa muhtasari wa maelezo yake hadi kufikia hapo kwa kusema: Tukio la Ghadir liliweka msingi wa kigezo na kielelezo cha utawala katika jamii ya Kiislamu na kusisitiza kwa kusema: Ukitoa kigezo cha Uimamu na Wilaya, Uislamu haukubaliani na tawala nyinginezo zozote, za kisultani, za watu binafsi, za kibeberu, za watu wanaopenda kujikumbizia kila kitu upande wao, za watu wenye viburi na za watu wanaofuata matamanio ya nafsi, anasa na ubwanyenye.
Vile vile amebainisha umuhimu wa kadhia ya Ghadir ambayo Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume Wake aitangaze na kwamba risala aliyetumwa kuifikisha hatakuwa ameifikisha kama hakutanga Uimamu na kuongeza kuwa: Itikadi hiyo ya Kiislamu imesimama juu ya msingi madhubuti wenye hoja zisizokanushika, lakini pamoja na hayo, wakati wa kuibainisha na kuitangaza itikadi hiyo, inabidi watu wawe macho, wasije wakaitumia kujeruhi hisia za Waislamu wa Kisuni, kwani kufanya hivyo ni kinyume na sira ya Maimamu maasumu (Alayhimus Salaam).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza tena na tena kuhusu umuhimu wa umoja na mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu na huku akigusia kwamba, kusema maneno yoyote yale mabaya dhidi ya shakhsia wakubwa na viongozi kwa Waislamu wa madhehebu mengine, kwa hakika ni kuzuia kufika misingi ya kimantiki na yenye hoja madhubuti ya Uimamu. Amesisitiza kuwa, kitendo chochote kile cha kuchochea hisia za watu wa madhehebu mengine ya Kiislamu kwa jina la Ushia, kwa hakika huo si Ushia halisi, bali huo ni Ushia wa Kiingereza na matokeo yake ni kujitokeza magenge khabithi na mamluki wa Marekani na wa shirika la kijasusi la Uingereza kama vile Daesh na Jabhatun Nusra ambayo yanafanya jinai na kusababisha hasara kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kuashiria sifa za kimaanawi na kiutu za Imam Ali AS kama vile kuwa na imani kubwa sana, kuwa wa mwanzo kuingia katika Uislamu, kujitolea kikamilifu katika njia ya Uislamu, ikhlasi, elimu, maarifa ya Allah, ushujaa, huruma, kujitolea na kusamehe na kuongeza kuwa: Sehemu nyingine ya sifa za aina yake za mtukufu huyo inahusiana na mbinu alizotumia katika kuongoza dola ya Kiislamu. Miongoni mwa sifa hizo ni uadilifu, insafu na kuwaweka daraja sawa wananchi wote, kujiweka mbali na anasa za kidunia, tadibiri, kutochelewesha hata kidogo kutekeleza majukumu, uwazi, kuiongoza jamii kuelekea kwenye taqwa na kufanya haraka sana katika kutenda haki na uadilifu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusiana na namna Imam Ali (Alayis Salaam) alivyojiepusha na anasa za dunia au kutumia utawala katika mambo yake binafsi na kusisitiza kwamba: Wasiwasi na ushawishi unaomkumba mtu, wa kutumia vibaya vyanzo vya fedha vilivyo mikononi mwake kujinufaisha binafsi, ni miongoni mwa mabalaa ambayo yanazitesa tawala zisizo za Mwenyezi Mungu, lakini utawala ambao kigezo na kielelezo chake ni Uimamu na Wilaya, unapinga vikali mambo kama hayo na unapiga marufuku kutumia mali ya umma kwa mambo ya watu binafsi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema: Imam Ali (Alayhis Salaam) alikuwa akifanya tadibiri sana katika kumjua rafiki na adui na katika kuwaainisha maadui na hayo yanaonekana wazi katika hatua zilizochukuliwa na mtukufu huyo kwenye vita vitatu alivyopigana na maadui baada ya kuwa kiongozi wa dola ya Kiislamu. Hatua hizo zinatofautiana kulingana na mazingira ya kila vita.
Amesema, Amirul Muminin Imam Ali (Alayhis Salaam) alikuwa ni shakhsia aliyekusanya sifa za kila upande, alikuwa shakhsia adhimu na ambaye ni vigumu kuzungumzia ipasavyo wasifu wake. Amesema, jukumu letu sisi ni kujitahidi kupiga hatua kuelekea kwenye kilele hicho na kustafidi ipasavyo na sifa zake hizo kwa kadiri ya uwezo na kiwango cha imani yetu.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia ulazima wa kujipamba Mashia kwa tabia na maadili ya Ahlul Bait AS na kusema: Mtu ambaye anapokea rushwa au anatumia "Baitul Maal" kwa manufaa yake binafsi au anayekodolea macho maovu na ambaye hana hisia zozote mbele ya wajibu wa kuiongoza vizuri jamii, mtu huyo si fakhari wala si pambo kwa Jamhuri ya Kiislamu wala kwa jamii ya Kiislamu, bali ni aibu kwa Mashia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, sisi kamwe hatuwezi kuishi kama alivyokuwa akiishi Imam Ali (Alayhis Salaam) kwa uchaji mkubwa mno wa Mwenyezi Mungu, lakini pamoja na hayo tunaweza kuingia kwenye mkondo wa njia hiyo iliyojaa nuru kwa kujiweka mbali na israfu na kuchupa mipaka. Aidha amesema: Inasikitisha kuona kuwa, jamii yetu imekumbwa na jambo la aibu la israfu na israfu nayo iko kwa sura nyingi miongoni mwake ni israfu katika maisha binafsi ya mtu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, moja ya madhara ya israfu katika jamii, ni kuharibu uchumi wa nchi. Ameongeza kuwa: Kama jamii inataka kuwa na nguvu za ndani za kiuchumi na kufikia daraja ya juu inayotakiwa, basi jamii hiyo haina njia nyingine ila kupambana na israfu.
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, jukumu la kwanza kabisa la wananchi ni kupambana na israfu na huku akisisitiza kuwa kushikamana na Wilaya na Uimamu wa Imam Ali AS inabidi kuonekane kivitendo amesema: Moja ya njia zinazotumiwa na adui kutoa pigo, ni kutumia udhaifu wa jamii, hivyo kuna wajibu wa kurekebishwa udhaifu wowote unaojitokeza.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesema, lengo kuu la adui hivi sasa ni kuvuruga uchumi wa Iran na huku akigusia namna ambavyo amekuwa akisisitizia mara kwa mara suala la kushikamana na uchumi wa kimuqawama amesema: Anachopigania adui ni kuharibu uchumi wa wananchi ili hatimaye wananchi hao wauchukuie Uislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Amesisitiza kuwa: Kwa kuzingatia hali hiyo, ni jukumu la Serikali, Bunge na maafisa wa sekta nyingine za wananchi kuwa na mipango mizuri ya kukabiliana na njama hizo za adui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na harakati nzuri za vijana wa Iran katika kuuhuisha Uislamu na kusimamisha dini na kusema, vijana hao kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu watampigisha magoti adui yeyote yule ikiwemo Marekani na utawala wa Kizayuni.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Sababu inayonifanya nisisitize mno katika maneno yangu kwamba nina mtazamo mzuri na matumaini ya mustakbali mwema ni kuweko vijana kama hawa na uhakika kama huu ambao unao uwezo wa kuifanya nchi isonge mbele.
Vile vile amesema, vijana walio imara kiimani, wenye msukumo wa hali ya juu na walio tayari wakati wote kuingia katika medani za jihadi na kulinda nchi, ni wengi nchini Iran. Amesisitiza kuwa: Huu ndio huo msukumo ambao utaweza kuiokoa nchi, hivyo kuna wajibu wa kuuimarisha na kuutia nguvu msukumo huo.