Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wajumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Kielimu
02/10/2016
Ayatollah KhameneiAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Jumapili) ameonana na wajumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Kielimu (vyuo vikuu vya kidini) na huku akisisitiza kuwa, Hawza za Kielimu haziwezi kutenganishwa kabisa na masuala ya serikali ya Kiislamu na kuongeza kuwa, serikali ya Kiislamu inaihitajia Hawza ya Kielimu yenye watu makini, walioiva kielimu, wasafi, wabunifu na wanaojua mahitaji ya kila leo duniani, kwa ajili ya kueneza mafundisho na sheria za Kiislamu katika upeo tofauti wa maisha ya mwanadamu na kuingia ndani kabisa ya jamii. Aidha amesema: Moja ya mahitaji makuu na muhimu ya Hawza ya Kielimu hivi sasa ni kubuni mpango wa mabadiliko katika Hawza na kuweka mipango ya muda mrefu, ya kina na ya kufanikishwa katika muda maalumu kulingana na mpango huo wa mabadiliko na malengo yaliyokusudiwa.
Amesisitiza kuwa, kuweka mipangilio mizuri katika Hawza ya Kielimu kwenye vitengo mbali mbali hususan kitendo cha masomo na uanachuo, utekelezaji wa masuala ya kiutawala inabidi yote yafanywe kwa ajili ya kusaidia na kulisha uhusiano na serikali ya Kiislamu. Ameongeza kuwa: Hawza ya Kielimu ni nguzo ya kusimamisha sheria na hukumu za Kiislamu, hivyo kama serikali ya Kiislamu itakuwa inatekeleza vilivyo sheria na hukumu za Kiislamu, jukumu la Hawza ya Kielimu ni kuiunga mkono serikali hiyo kwa nguvu zake zote na kuionya serikali hiyo kila inapofanya makosa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, ni jambo la dharura mno kwa Hawza ya Kielimu kuwa na mipango ya muda mrefu na kusisitiza kuwa: Katika mipango hiyo, inabidi malengo yawekwe wazi kikamilifu na yawe yana sifa ya ya kutekelezeka. Yawe na muda maalumu wa kuyafanikisha kwa namna ambayo mipango hiyo iweze kutathminiwa vizuri na kufanyiwa mabadiliko kila inapohitajika.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, mipango ya muda mrefu ya Hawza inabidi isimame juu ya mpango wa mabadiliko makuu ya Hawza na kuongeza kuwa: Inabidi kuanzishwe kituo kikuu cha utafiti wa kiistratijia kitakachoundwa na watu muhimu na walioiva katika Hawza; na ndani ya kituo hicho ndimo mupatikane mipango ya mabadiliko na mipango mingine mbalimbali ya kiistratijia.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei ametoa nasaha kadhaa akisema: Kujiepusha na mifumo ya kiutawala inayofanana na serikali, kuweko vikao na mazungumzo baina ya wakuu wa Hawza na wanafunzi, kuleta anga ya kuwa karibu mno na Qur'ani Tukufu kati ya wanafunzi, kugundua vipaji bora na kuvilea ipasavyo, kueneza tabia ya kutalii na kusoma hususan katika nyuga za historia na tafsiri, kulea wafanya tablighi kwa njia ya kalamu, hotuba na tablighi kwa kutumia Intaneti ni miongoni mwa nukta ambazo zinapaswa kupewa umuhimu mkubwa katika Hawza za Kielimu.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ustadi, Katibu wa Baraza Kuu la Hawza za Kielimu, ametoa ripoti fupi kuhusu mipango na kazi za baraza hilo na changamoto zilizoko mbele yake.
Vile vile Hujjatul Islam Walmuslimin A'rafi, mkuu wa Hawza za Kielimu ametoa ufafanuzi kuhusu hatua muhimu mno zilizochukliwa katika miaka ya hivi karibuni katika vitengo mbali mbali vya Hawza za Kiaelimu.