Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Makamanda wa Jeshi la Polisi
04/10/2016
Without Security, Economics, Culture and Public Services Cannot Be PursuedAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo adhuhuri (Jumanne) ameonana na makamanda na maafisa wa jeshi la polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mnasaba wa siku ya jeshi hilo na kusema kuwa, suala la usalama ni moja ya nguzo kuu na za kimsingi za maendeleo ya nchi. Aidha amesisitizia nafasi muhimu ya jeshi la polisi katika kuleta na kudumisha amani na kuongeza kuwa, kuna wajibu wa kuongezwa siku baada ya siku uwezo na utayari wa jeshi la polisi pamoja na azma na imani ya wafanyakazi wake.
Katika mkutano huo, Ayatullah Udhma Khamenei amesema pia kuwa, usalama una maana ya utulivu wa kisaikolojia wa watu mmoja mmoja na wa jamii nzima na kuongeza kuwa: Wakati usalama unapokosekana, uwezekano wa kufanyika harakati mbali mbali za kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa na utoaji huduma nazo hupoteka hata kama katika jamii kutakuwa na uwezo na msukumo unaotakiwa kati ya watu wa jamii hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ushahidi kutoka katika Qur'ani Tukufu ili kuthibitisha kuwa usalama huwa sababu ya kuongezeka imani ya waumini. Aidha amesema: Jeshi la polisi ni moja ya nguzo muhimu zaidi za usalama nchini. Amesema, ni jambo lisilo na shaka kwamba nguzo hiyo adhimu ya usalama ina nguvukazi za watu ambao wengi wao ni makini, watu wema na wanaofanya kazi kwa ikhlasi na bidii kubwa, na inabidi nia, imani, msukumo na moyo huo ulindwe daima kwenye jeshi hilo.
Vile vile amegusia kazi kubwa inayofanywa na jeshi la polisi nchini Iran na kuhimiza kupewa mazingatio maalumu nafasi ya vituo vya polisi kutokana na kazi yao ya kukabiliana moja kwa moja na watu wa aina mbali mbali katika jamii.
Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia mabadiliko ya haraka yanayotokea katika sekta mbali mbali kama vile sekta ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, ulazima wa kuongeza utayari na kuufanya wa kisasa uwezo wake jeshi hilo, kuelewa majukumu na kuyatekeleza kikamilifu pamoja na kutumia vyombo vya habari kubainisha kwa umakini na kwa kina kazi na huduma zinazotolewa na jeshi la polisi kwa wananchi, ni mambo muhimu kwa ajili ya kudhamini na kuimarisha usalama nchini.
Kabla ya mkutano huo, hadhirina wamesalishwa sala za Adhuhuri na Laasiri na Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.