Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Rais wa Finland
26/10/2016
Terrorism is not only ISIS, Saudi crimes are the worst type of terrorismAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo (Jumatano) ameonana na Rais Sauli Niinistö wa Finland na huku akizungumzia kadhia ya ugaidi ambayo ni moja ya masaibu machungu ya jamii ya mwanadamu leo hii amesema kuwa, kuua watu kwa umati kama vile kuuliwa kwa halaiki wananchi wa Yemen ni katika ugaidi mbaya kabisa. Amesisitiza kwamba, kazi ya kupambana na ugaidi inahitajia nia ya kweli ya watu wote wenye ushawishi ndani ya madola ya kimataifa na watu wenye busara duniani pamoja na tawala na madola yenye heshima ulimwenguni wote kwa pamoja wanapaswa kuchukua yatua za kweli kupambana na jambo hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameyataja matamshi na vitendo vya Marekani na baadhi ya tawala zinazojidai kupambana na ugaidi, si wakweli katika madai yao hayo na kuongeza kuwa: Tawala zote hizo zinazingatia tu maslahi yao binafsi na hazifikirii kabisa kuangamiza ugonjwa wa ugaidi si nchini Iraq na si nchini Syria.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mfano wa namna madola hayo yasivyo wakweli katika vita dhidi ya ugaidi kwa kuzungumzia mauaji ya umati yanayofanywa dhidi ya wananchi madhlumu wa Yemen na kusema: Ugaidi hauishii tu kwenye vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na magenge yasiyo rasmi, lakini kitendo cha baadhi ya nchi cha kuwaua kwa umati watu wasio na hatia kama vile mashambulizi ya Saudia dhidi ya watu waliokuwa wamekusanyika mazikoni nchini Yemen na yaliyopelekea mamia ya watu kuuawa na kujeruhiwa, ni katika ugaidi mbaya zaidi ambapo licha ya kupita mwaka mmoja na miezi saba ya vitendo kama hivyo huko Yemen, lakini hadi leo hii hakuonekani nia ya kweli ya kukabiliana na ugaidi huo.
Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu utatuzi wa mgogoro wa Syria nao ni wa kimantiki uliosimama juu ya msingi wa kulinda haki za wananchi na serikali hali ya nchi hiyo. Ameongeza kuwa: Marekani na baadhi ya nchi zinashinikiza kuondolewa madarakani serikali ya Syria wakati ambapo jambo la wajibu hapa ni kutangazwa kwanza walioanzisha vita hivyo na sababu za kuendelea kwake (ili iwezekane kumaliza vita hivyo).
Amekumbusha kuwa, kitendo cha Umoja wa Mataifa cha kukataa kumkiri muanzishaji vita ndicho kilichopelekea kudumu muda mrefu vita vilivyoanzishwa na utawala wa Saddam dhidi ya Iran. Aidha amesema: Tab'an miaka michache baada ya vita hivyo ilivyolazimishwa Iran kupigana, Katibu Mkuu wa wakati huo wa Umoja wa Mataifa ambaye alikuwa mtu wenye nafsi yenye kujuta na shujaa, alitangaza hadharani kwamba, Saddam ndiye aliyeanzisha vita hivyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amekosoa pia misimamo ya Katibu Mkuu wa hivi sasa wa Umoja wa Mataifa na kusema: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anathubutu kutangaza hadharani kuwa, kutokana na fedha unazopatiwa umoja huo na Saudi Arabia, kamwe hauwezi kulaani mauaji wa watoto wadogo yanayofanywa na Saudia huko Yemen, suala ambalo linaonesha hali ya kusikitisha sana ya kimaadili waliyo nayo wanasiasa wa kimataifa na tunatumai Katibu Mkuu ajaye wa Umoja wa Mataifa ataweza kushika nafasi hiyo akiwa mtu huru.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amekaribisha juhudi za kustawishwa uhusiano baina ya Iran na Finland na kusisitiza kuwa: Maelewano yaliyotiwa saini baina ya serikali za nchi hizi mbili inabidi yatekelezwe kivitendo kwani kama hayakutekelezwa, yataleta sura mbaya kwa wananchi.
Katika mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Sauli Niinistö wa Finland ameelezea kufurahishwa kwake na mazungumzo aliyofanya na viongozi wa Iran na kusema kuwa: Leo kumetiwa saini hati nne za maelewano katika nyuga tofauti kama ambavyo kumepigwa hatua nzuri pia katika mazungumzo baina ya timu za kibiashara za nchi mbili.
Aidha amemshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa msimamo wake kuhusu suala zima la kupambana na ugaidi na kusema, tawala za nchi mbali mbali pamoja na Umoja wa Mataifa zimeshindwa kupambana na ugaidi. Ameelezea kusikitishwa kwake na wimbi la wakimbizi kutoka nchi kama za Syria, Iraq na Yemen na jinsi watoto wengi walivyouawa pamoja na mama zao katika mashambulizi ya kigaidi na kuongeza kuwa, dunia ya leo imejaa machafuko.
Vile vile amegusia nafasi muhimu ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati na mchango wake mkubwa katika kupambana na ugaidi na kusisitiza kwa kusema: Iran imefanya jitihada zake zote kwa ajili ya kutokomeza vitendo vya ugaidi na nina yakini jambo hilo litaendelea.