Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Rais wa Slovenia
22/11/2016
Slovanian president meets with LeaderAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo jioni (Jumanne) ameonana na Rais Borut Pahor wa Slovenia na huku akiashiria matukio machungu na ya kuhuzunisha yanayojiri hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati na nafasi ya baadhi ya madola makubwa ya kupandikiza hali ya ukosefu wa utulivu na vita katika eneo hili amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima inatoa mwito kwa nchi huru duniani kushiriki vilivyo kukabiliana na mashinikizo yanayoyakumba mataifa ya dunia na inazitaka nchi hizo zisinyamazie kimya na kuangalia kwa macho tu jambo hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, mapigano ya kutumia mabavu yaliyoko hivi sasa katika nchi za eneo la magharibi mwa Asia na kuzuka magenge ya kigaidi kama vile Daesh ni matunda ya uingiliaji na uchochezi wa baadhi ya madola makubwa na kuongeza kuwa, jukumu la nchi huru duniani ni kufanya juhudi za kuzima moto wa mapigano hayo na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, tofauti kabisa na propaganda za madola ya kibeberu, inapigania jambo hilo hilo na kamwe haiingilii masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja muungano wa Wamarekani dhidi ya genge la Daesh kuwa ni muungano uliofeli na huku akibainisha sababu za kufeli huko amegusia mitazamo mwili iliyopo kuhusu suala hilo na kusema kuwa, kwa mujibu wa mtazamo wa kwanza, Wamarekani hawana nia wala ratiba kabisa ya kulimaliza kundi la Daesh na wanatekeleza siasa za Uingereza wakati ilipokuwa inaikoloni India, ambapo ililifanya eneo la Kashmir kuwa eneo la kugombaniwa milele baina ya India na Pakistan na hadi leo hii nchi hizo mbili zina matatizo kuhusu eneo hilo. Amesema, kwa mtazamo huo wa kwanza, hali ni hiyo hiyo kwa upande wa genge la Daesh, Wamarekani wanafanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa genge hilo halimalizwi katika nchi za Iraq na Syria.
Ameongeza kuwa: Kwa mujibu wa mtazamo wa pili, Wamarekani wana nia ya kutatua suala la Daesh lakini mbinu wanazotumia si sahihi. Tab'an matokeo ya mitazamo yote hiyo miwili ni kuwa hivi sasa mwaka mzima umepita na leo hii Iraq, lakini zaidi Syria, zina hali mbaya na ya kuumiza sana.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia madhara ya kuzushwa machafuko na ukosefu wa utulivu katika nchi za magharibi mwa Asia ikiwa ni pamoja na wimbi la wakimbizi na kusema kuwa, katika hali ambayo nchi za Ulaya zimeshindwa kuvumilia kuingia barani humo angalau wakimbizi elfu mbili tu, Iran kwa miaka mingi sasa ni mwenyeji wa karibu wakimbizi milioni tatu kutoka Afghanistan na imewadhaminia mazingira mazuri ya kuishi kwa amani na kupata elimu na kuamiliana nao kwa kifua kipana na kibinadamu kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia mashambulizi ya mwaka mmoja na miezi minane sasa yanayofanywa na Saudi Arabia dhidi ya wananchi wa Yemen na kuangamizwa miundombinu yote nchini humo na kusema kuwa, hilo ni jambo jengine chungu na linaloumiza nyoyo lililolikumba aneo hili hivi sasa. Ameongeza kuwa: Nchi huru duniani zina wajibu wa kusimama imara kukabiliana na jambo hilo kwani kuliweka kwenye mashinikizo taifa la watu, kwa kweli ni maumivu na ni mateso kwa wanadamu wote.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amegusia uwezo mbali mbali wa Iran na Slovenia wa kuziwezesha nchi hizo mbili kushirikiana katika nyuga nyingi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amezungumzia namna Iran ilivyotekeleza kikamilifu ahadi zake katika makubaliano ya nyumklia na namna pande nyingine zilivyoshindwa kutekeleza ipasavyo majukumu yao kulingana na makubaliano hayo.
Katika mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Borut Pahor wa Slovenia amesema kwamba mazungumzo yake na viongozi wa Iran yalikuwa mazuri sana. Amesema, nchi yake inafuatilia njia za kuimarisha uhusiano wake na Iran katika nyuga zote. Vile vile amesema, Iran ni nguzo ya utulivu na usalama katika eneo hili na ni nchi inayostahiki kuheshimiwa. Vile vile ameisifu Iran kwa namna ilivyoendesha mazungumzo ya nyuklia na vile vile maendeleo makubwa iliyopata katika miaka ya hivi karibuni na kusema kuwa Slovenia na Iran zina tajiriba nyingi za pamoja na zina nyuga chungu nzima za kuweza kuimarisha uhusiano baina yao.