Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Mabasiji
23/11/2016
Basij commanders and forces meet with Ayatollah KhameneiAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatano) ameonana na maelfu ya mabasiji na kusema kuwa, Basiji ni "Jeshi la Mapinduzi" na "dhihirisho la demokrasia ya kidini" lililoegemea kwenye nguzo ya busuri na muono wa mbali. Vile vile amesisitizia ulazima wa kuweko mipango mizuri ya kina inayotumia mbinu ya kuunda timu za kifikra za kuongeza nguvu na uimara wa Basiji zitakazoliwezesha jeshi hilo la kujitolea kushiriki vilivyo na kwa faida kubwa zaidi katika nyuga tofauti za jamii.
Vile vile amesema: Moyo wa Basiji una maana ya kuona kwamba Mwenyezi Mungu yuko pamoja nawe muda wote, kutokata tamaa, kuwa mchangamfu muda wote na kutokwamishwa na chochote, hivyo tunawajibu watu wenye nyoyo dhaifu, waliokata tamaa na wanaomuogopa adui na kuathiriwa vibaya na fikra ya kujiona duni na kudhani hawawezi kufanya lolote kwamba, kwa kutegemea nguvu za Mwenyezi Mungu na kuamini mchango mkubwa wa wananchi, tunaweza kuyashinda matatizo yote bila ya kuliogopa dola lolote lile.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema hayo wakati alipoonana na makamanda wa jeshi la Basiji, na huku akigusia hatua ya Baraza la Kongresi la Marekani ya kurefusha vikwazo dhidi ya Iran kwa miaka kumi zaidi amesema kwamba, serikali ya hivi sasa ya Marekani imefanya ukiukaji mkubwa sana wa makubaliano ya nyuklia na miongoni mwake ni kurefushwa vikwazo hivyo dhidi ya Iran kwa miaka kumi zaidi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kama vikwazo hivyo vitatekelezwa kivitendo, bila ya shaka yoyote utakuwa ni uvunjaji wa makubaliano ya JCPOA na Wamarekani wajue kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itajibu jambo hilo.
Vile vile ameashiria matamshi ya viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu na wasimamiaji wa makubaliano ya JCPOA ambao walisema kuwa, lengo la makubaliano hayo ya nyuklia ni kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran na kuongeza kuwa, makubaliano ya nyuklia yaani JCPOA hayapaswi kutumiwa kabisa kama mashinikizo dhidi ya taifa na nchi ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia masuala yanayozihusu Iran na serikali ya Marekani na kusema kuwa: Sisi hivi sasa hatuwezi kusema lolote kuhusiana na serikali mpya inayosubiriwa kuingia madarakani huko Marekani.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, Iran hailiogopi dola lolote duniani kutokana na imani yake kwa Mwenyezi Mungu na kwa kutegemea nguvu za wananchi wake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amezungumzia kufanyika kwa mafanikio makubwa matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein AS na kuongeza kuwa: Kushiriki mamilioni ya watu kwenye matembezi hayo kunaonesha mapenzi, mvuto pamoja na muono wa mbali walio nao maashiki hao wa Imam Hussein AS.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amewashukuru sana wananchi wa Iraq kwa kujitolea kwa mapenzi makubwa kuwahudumia wageni wa Imam Hussein AS na kutoa tahadhari akisema, kuna baadhi ya watu wana nia ya kuifuta na kuipotosha Arubaini ya Imam Hussein AS lakini hawatafanikiwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia jinsi nchi nyingine za eneo hili zilivyochukua kigezo cha Basiji katika mambo yao mbalimbali na jinsi adui anavyofanya njama za kutoa pigo kwa kigezo hicho muhimu na kuongeza kuwa, moja ya njama za adui ni suala muhimu mno la kujipenyeza ndani ya jamii ya Iran jambo ambalo nimekuwa nikilitolea tahadhari kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.