Kiongozi Muadhamu Aonana na Viongozi wa Nchi na Wageni wa Mkutano wa Umoja wa Kiislamu
17/12/2016
Govt officials and participants in Islamic Unity Conference met with Ayatollah KhameneiAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Jumamosi) ameonana na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wageni wa Mkutano wa 30 wa Umoja wa Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu pamoja na matabaka mbali mbali ya wananchi na kusisitiza kuwa, leo hii kuna irada mbili zinakabiliana katika eneo hili ambazo ni "irada ya mshikamano" na "irada ya mfarakano" na katika hali hii nyeti, kuitegemea Qur'ani Tukufu na mafundisho ya Mwenyezi na Mtume Mtukufu (Swallallahu Alayhi Waalihi Wasallam) ndiyo dawa ya kuleta mshikamano na umoja na kutatua matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa maulid matukufu ya Mtume wa Mwisho, Muhammad bin Abdullah (Swallallahu Alayhi Waalihi Wasallam) na maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Imam Jafar Sadiq (Alayhis Salaam) na kuongeza kwamba: Umuhimu wa uwepo mtakatifu wa Mtume wa Uislamu unaonekana katika mshikamano wa umma wa Kiislamu. Amesema: Mwenyezi Mungu Mtukufu anajifakharisha mbele ya wanadamu kwa kuwatumia neema kama hiyo ya Bwana Mtume Muhammad SAW ambayo haina mfano wake.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ushahidi kutoka ndani ya Qur'ani Tukufu inayomtaja Bwana Mtume Muhammad (Swallallahu Alayhi Waalihi Wasallam) kuwa ni rehema kwa viumbe wote na kusema kuwa, mafundisho ya Bwana Mtume SAW ndiyo njia ya kuwaokoa wanadamu wote. Ameongeza kuwa: Maadui wa wanadamu, mabeberu na waistikbari wanapinga mafundisho hayo matukufu na ni kwa sababu hiyo ndio maana Mwenyezi Mungu alimwamrisha Bwana Mtume (Swallallahu Alayhi Waalihi Wasallam) kwamba sambamba na kutowafuata wala kupatana na makafiri na wanafiki, asimame imara kupigana nao jihadi.
Ameongeza kuwa, kupigana jihadi dhidi ya maadui wa Uislamu na ubinadamu, ni jambo la wajibu na tab'an jihadi hiyo inaweza kufanyika kwa kuzingatia hali zake tofauti, baadhi ya wakati kwa kutumia nguvu za kijeshi, baadhi ya wakati kisiasa na baadhi ya wakati kiutamaduni bali hata kielimu na kwamba mataifa ya Waislamu na hususan mubalighina wa kidini na vijana wanapaswa kufanya utafiti wa kina na kuyaelewa vizuri na kiundani mafundisho ya Mwenyezi Mungu kuhusiana na Bwana Mtume Muhammad SAW na kuyatunmia kwa faida ya wanadamu wote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbushia njama za kila leo zinazofanywa na mabeberu na wakoloni, za kuzusha mizozo na mifarakano na kuwadhoofisha Waislamu na kuongeza kuwa: Ulimwengu wa Kiislamu leo hii umekumbwa na matatizo na mashaka mengi, na utatuzi pekee wa matatizo hayo ni umoja, ushirikiano, mshikamano na kuweka pembeni hitilafu za kimadhehebau na kifikra na kushikamana na mambo mengi mno yanayouunganisha umma wa Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Iwapo mataifa na tawala za nchi za Waislamu zitaungana, basi Wamarekani na Wazayuni kamwe hawawezi kupata nguvu za kuwabebesha Waislamu matakwa yao na njama ya kujaribu kuisahaulisha kadhia ya Palestina, nazo itashindwa.
Amesema, mauaji yanayofanywa dhidi ya Waislamu kuanzia Myanmar, mashariki mwa Asia, hadi Nigera, magharibi mwa Afrika na kupigana Waislamu katika eneo muhimu mno la magharibi mwa Asia yote hayo ni matokeo ya njama za waistikbari za kuzusha mizozo na mifarakano katika safu za Waislamu na kuongeza kuwa: Katika hali na mazingira kama hayo, Mashia wa Kiingereza na Masuni wa Kimarekani ni sawa na pande mbili za makali za mkasi zinazochochea moto wa mizozo na hitilafu katika umma wa Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amezitaja siasa na vitendo vya Waingereza katika kipindi cha karne mbili zilizopita kuwa chanzo cha shari na nakama kwa mataifa ya eneo hili na kusisitiza kuwa: Siku za hivi karibuni, viongozi wa Uingereza wakiwa wamekosa haya usoni wameituhumu Iran madhlumu na azizi kuwa eti ni tishio kwenye eneo hili wakati watu wote wanajua kwamba, kinyume kabisa na madai hayo, ni Waingereza ndio ambao daima wamekuwa tishio na chanzo cha ufisadi, hatari na nakama kwa mataifa ya eneo hili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuongezeka vitendo vya mabeberu vilivyo dhidi ya Uislamu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran kuwa linathibitisha namna waistikbari hao walivyo na woga wa kusimamishwa na kuendelea kuwepo mfumo wa Kiislamu wenye nguvu, wenye ustawi na ulio kigezo kwa mataifa mengine. Ameongeza kuwa: Hata kama maadui watajifanya wapole na kufanya mabadiliko katika dhahiri yao lakini batini yao ni ya kikatili na kihayawani kikamilifu na mataifa yote yanapaswa kujiandaa kukabiliana na maadui hao wasio na maadili wala dini wala insafu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameutaja umoja na mshikamano kuwa ndiyo njia bora kabisa ya kujiandaa kukabiliana na adui huyo inayohitajiwa na ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Makundi yote ya Kiislamu, yawe ya Kishia au ya Kisuni, yote yanapaswa kujiweka mbali na mifarakano na kuwepo Bwana Mtume Muhammad (Swallallahu Alayhi Waalihi Wasallam) na Qur'ani Tukufu na Kibla kimoja, viwe ni vitu vya kuwaunganisha na kuimarisha umoja na mshikamano wao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka Waislamu na serikali zao kuwa macho mbele ya ushetani na ushari wa mabeberu na kuhoji kwa kusema, kwa nini nchi ambazo zinaonekana za Kiislamu zinaleweshwa na maneno ya maadui kuhusiana na vitisho na uadui wa ndani ya ulimwengu wa Kiislamu na zinafuata waziwazi siasa za maadui hao wa umma mzima wa Kiislamu?
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei, amelitaka taifa la Iran lililopasi mtihani wake, kuendelea na njia iliyojaa fakhari ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) na ya Mapinduzi ya Kiislamu, kusimama imara kukabiliana na maadui na kuilinda na kuipigania haki bila ya kumuogopa mtu yeyote na kusema kuwa, bila ya shaka hiyo ndiyo siri ya kupata heshima, ustawi na ufanisi wa duniani na Akhera.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa hotuba fupi na sambamba na kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa maulid yaliyojaa nuru ya Bwana Mtume Muhammad (Swallallahu Alayhi Waalihi Wasallam) na mjukuu wake Imam Jafar Sadiq AS amesema, sira ya Mtume Mtukufu (Swallallahu Alayhi Waalihi Wasallam) haikuwa njia ya kati baina ya haki na batili bali alichagua kikamilifu njia ya haki na hii ndiyo maana ya kuweka mlingano mzuri katika mambo.
Mwishoni mwa mkutano huo, wageni mbali mbali wa mkutano wa Umoja wa Kiislamu wameweza kuonana na kuzungumza kwa karibu na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.